1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga astaafu rasmi

12 Januari 2021

Kenya inaufungua ukurasa mpya baada ya Jaji Mkuu David Kenani Maraga kustaafu rasmi siku ya Jumatatu. Jaji Maraga anastaafu baada ya kufanya kazi kwa miaka minne na kutimiza umri wa miaka 70 ambao ni kikomo cha mtu kuhudumu kama jaji mkuu kwa mujibu wa katiba ya Kenya.

https://p.dw.com/p/3nn3k

Atakumbukwa kwa kusukuma matumizi ya teknolojia kwenye idara ya mahakama na ujenzi wa majengo mapya 22 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Kwa sasa Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu anakaimu nafasi hiyo hadi mwengine atakapoteuliwa. 

Muda mfupi baada ya saa tano asubuhi leo Jumatatu, David Maraga alimkabidhi rasmi naibu wake Philomena Mwilu magwanda na vyombo vya dola vya uongozi wa mahakama nchini Kenya.

Kwenye hotuba yake ya mwisho, jaji mkuu wa zamani David Maraga alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa fursa kuhudumu kwenye idara ya mahakama kwa miaka 18 kwa jumla akiwa na majukumu tofauti.

Hafla hiyo iliyofanyika nje ya majengo ya Mahakama ya Juu iliwaleta pamoja viongozi wa kidini, wanasheria, mawakili na familia yake.

Jaji mwenye msimamo mkali na imani ya dini 

David Maraga atakumbukwa kwa msimamo wake wa kufuata dini na kukataa kata kata kusikiliza kesi zozote siku ya Jumamosi ambayo ni ya ibada kwa waumini wa kanisa la Sabato.

Aliishukuru familia yake kwa kusimama naye kila wakati hata alipokwaruzana na uongozi wa taifa kwa msimamo wake wa kushikilia ukweli. 

Kufuatia tukio la leo, naibu jaji mkuu Philomena Mbete Mwilu anakaimu nafasi hiyo hadi atakapoteuliwa mwengine.

Kwenye hotuba yake baada ya kukabidhiwa rasmi wadhifa huo, Jaji Mwilu alimsifu mtangulizi wake kwa uongozi usiokuwa na mfano.

Mrithi wa Maraga kuwa mwanamke? 

Ifahamike kuwa Jaji Mwilu ni mwanamke wa kwanza kuwahi kushika nafasi ya jaji mkuu. Itakumbukwa kuwa Jaji Mwilu ni mmoja ya waliosikiliza kesi ya matokeo ya uchaguzi wa raisi mwaka 2017 iliyoufutilia mbali ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Majaji wengine waliosikiliza kesi hiyo ni Jaji Mkuu mstaafu David Maraga, Jaji Smokin Wanjala na Isaac Lenaola.

Kenia Philomena Mwilu ARCHIV
Kaimu Jaji Mkuu wa Kenya, Philomena Mwilu (katikati) akiteta na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga (kulia)Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Philomena Mwilu na majaji wengine watano walikosa kufika mahakamani pale kesi lipowasilishwa kuzuia uchaguzi wa pili wa rais.

Mwezi uliopita, mwanaharakati Okiya Omtata alifika mahakamani kupinga na kuzuia uteuzi wa Jaji Mwilu kukaimu nafasi ya jaji mkuu kwa sababu ya tuhuma za ufisadi zinazomuandama.

Kufikia sasa mahakama haijatoa kauli yake ya mwisho. Jaji mkuu mstaafu aliijaza nafasi iliyoachwa wazi na Dokta Willy Mutunga aliyestaafu mwezi Juni mwaka 2016.

Kabla ya kuwa jaji mkuu mwezi Juni mwaka huo huo, David Maraga aliwahi kuwa kiongozi wa mahakama ya rufaa ya Kisumu na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya idara ya mahakama.

Kadhalika alihudumu kama jaji kwenye mahakama za Nakuru na Nairobi.