Jaji Ugiriki awaachia huru watuhumiwa wa kuzamisha meli
21 Mei 2024Wanaume hao walipandishwa kizimbani hivi leo katika mji wa Kalamata, kusini mwa Ugiriki walidaiwa pia kuwaua mamia ya wahamiaji na kuibua hofu na wasiwasi kuhusu operesheni dhidi ya waomba hifadhi na ulinzi wa mipaka ya Umoja wa Ulaya.
Muda mfupi baada ya kesi hiyo kuanza mwendesha mashatka wa serikali Ekaterini Tsironi alisema Ugiriki haina mamlaka ya kuendesha kesi hiyo na akapendekeza ifutuliwe mbali akisema meli hiyo iliyokuwa imejaa kupindukia ilizama katika eneo la pwani lililo nje ya himaya ya Ugiriki.
Washtakiwa, wengi wao wakiwa katika umri wa miaka 20, walikabiliwa na kifungo cha hadi maisha jela iwapo wangetiwa hatiani kwa mashitaka kadhaa ya uhalifu kwa kuzama kwa meli ya uvuvi kwa jina "Adriana" mnamo Juni 14 mwaka uliopita.
Zaidi ya watu 500 wanaaminiwa walizama pamoja na meli hiyo ambayo ilikuwa ikisafiri kutoka Libya kuelekea Italia.