Jamii ya kimataifa yatoa wito wa amani Israel na Gaza
13 Mei 2021Hii ni baada ya kuzuka kwa machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo kwa miaka takribani saba.
Roketi moja lililorushwa kutoka Palestina limeanguka katika jengo katika mji mkuu wa kibiashara wa Israel Tel Aviv na kulingana na polisi Waisraeli watano wamejeruhiwa. Ving'ora vimesikika kote katika miji ya kusini mwa Israel na kuwapelekea maelfu kukimbia kuyanusuru maisha yao.
Katika mashambulizi mapya leo, Israel imeharibu jengo moja la makaazi katikati mwa mji wa Gaza. Mtu mmoja ameuwawa na kombora la Israel kusini mwa Gaza. Mashambulizi ya Israel pia yameliangusha jengo la kituo cha televisheni cha Palestina Al-Aqsa kilichoanzishwa na Hamas.
Njia ya pekee ya kusitisha vifo ni mashambulizi kusitishwa
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema amezungumza na rais wa Palestina Mahmud Abbas akitaka kusitishwa kwa mashambulizi hayo ya angani. Naye waziri wa Uingereza kuhusiana na masuala ya Mashariki ya Kati james Cleverly ametoa wito huo huo wa amani.
"Gaza ni mojawapo ya maeneo yaliyo na watu wengi zaidi duniani. Ukweli ni kwamba, njia ya pekee wanayoweza kupunguza vifo ni mashambulizi kusitishwa. Na ndio maana tunataka Hamas iache kurusha roketi. Na tunatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili Israel nayo isifikirie kufanya mashambulizi ya kijeshi Gaza," alisema Cleverly.
Wakati mashambulizi hayo ya angani yakiendelea, machafuko kati ya Waarabu na Waisraeli yameripotiwa ndani ya Israel.
Usiku wa kuamkia leo, makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia kote Israel yameingia mitaani na kupambana na maafisa wa usalama na Waisraeli wenye asili ya Kiarabu. Polisi inasema ilifahamishwa kuhusiana na machafuko aktika miji kadhaa ikiwemo Lod, Acre na Haifa na kuthibitisha kuwakamata watu 374 muda mfupi baada ya saa sita usiku.
Hali ya dharura katika mji ulio na mchanganyiko wa Wayahudi na Waarabu wa Lod
Televisheni ya Israel imeonyesha ukanda wa video ambapo kundi la Waisraeli limempiga mtu anayesemekana kwamba ni Mwarabu hadi akapoteza fahamu katika eneo la Bat Yam karibu na Tel Aviv.
Hali ya dharura imetangazwa katika mji ulio na mchanganyiko wa Wayahudi na Waarabu wa Lod ambapo sinagogi na mali zengine za Kiyahudi zimechomwa na raia mmoja wa Kiarabu kuuwawa kwa kupigwa risasi.
Israel imeandaa vikosi vya majeshi ya ardhini katika mpaka wa Gaza na kulingana na msemaji wa jeshi, wako katika hatua za kuandaa operesheni za ardhini. Hatua hii inakumbusha yale yaliyofanyika katika vita vya Israel na Gaza mwaka 2014 na 2008 hadi 2009.
Maafisa wa afya Gaza wanasema wanachunguza vifo vya watu kadhaa usiku wa kuamkia leo ambao wanasema huenda ikawa walivuta gesi ya sumu. Kwa sasa uchunguzi bado unaendelea na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusiana na hilo.