Janga la Covid-19 laendelea kuitikisa dunia
14 Mei 2021Waziri mkuu wa India Narendra Modi amewatahadharisha wananchi kuchukua hatua za ziada za tahadhari wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mripuko mbaya wa kirusi cha Corona kinachosambaa kwa kasi kubwa.
Modi ametoa tahadhari zaidi kwa wakaazi wa vijijini ambako ndiko wanakoishi kiasi thuluthi mbili ya wakaazi takriban bilioni 1.4 wa nchi hiyo.Amewatolea mwito wakaazi wa vijijini,mabaraza ya vijijini na serikali kushirikiana kukabiliana na changamoto hioy.
Lakini pia amesema jeshi la ulinzi,vikosi vya jeshi la wanamaji na angani wamejiunga na mapambano hayo dhidi ya janga hili la kiafya nchini humo.
Akihutubia mkutano wa jukwaa la wakulima hii leo amesema watu wamepoteza watu wao wa karibu na anafahamu uchungu wa watu wanaoteseka.
Visa vya maambukizi vyaongezeka huku porojo kuhusu Covid-19 zashamiri
Wizara ya afya nchini humo leo imeripoti visa 343,144 vipya vya maambukizi vilivyorikediwa katika kipindi cha saa 24,idadi hiyo ikionesha kupungua kidogo kwa maambukizi ikilinganishwa na siku moja kabla ya hapo.
Lakini pia wizara imeeleza kwamba watu 4000 wamekufa katika muda huo wa saa 24.
Na kufikia sasa kwa ujumla waliokufa nchini humo ni watu 262,317. Kadhalika aina mpya ya kirusi kinachosambaa kwa kasi katika taifa hilo la Kusini mwa Asia, kinaelezwa pia kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.
Lakini pia inaelezwa kwamba kuna ongezeko la visa vya kusambaza taarifa za uwongo kuhusu janga hili.
Mifano mingi imetolewa ikiwemo vidio inayosambaa kwenye mtandao wa whattsap ukiomuonesha mtu anayenadi kwamba tone moja la maji ya limao ukilitia puani basi utaimaliza Covid-19 kwa sekunde tano tu.
Mtu anayenadi uwongo huo kavaa nguo za kiasili za kidini na anasema tone la maji ya limao ni kama chanjo. Lakini pia inaelezwa kuna porojo chungunzima za kutisha zinazoenezwa kuhusu athari ya chanjo huko India.
China yashambuliwa kwa kutumia chanjo kidiplomasia
Kirusi cha Corona aina ya B.1.617 kinachosambaa India mpaka sasa kimegundulika katika nchi nane za bara la Amerika ikiwemo Canada na Marekani.
Hayo yameelezwa na Jairo Mendez mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka shirika la afya duniani WHO. Huko Taiwan wakaazi wametolewa mwito wa kupakua App maalum ya mtandao inayomuonesha mtu umbali anaotakiwa kukaa kuzuia maambukizi.
Ni baada ya kisiwa hicho kurekodi visa 29 vya maambukizo ya ndani kwa siku.
Kwa upande mwingine Marekani pamoja na Honduras zimekosoa kitendo cha suala la chanjo ya Covid-19 kutumiwa kisiasa,baada ya Taiwan kuishambulia China kwa kutaka kutumia suala hilo la chanjo kumvutia kidiplomasia mmoja wa washirika wa Taipei.
Honduras ni miongoni mwa nchi ndogo za Amerika ya Kusini ambayo bado ina uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan,sasa nchi hiyo imesema inafikiria kufungua ofisi China ili iweze kupata chanjo ya Covid-19 inayoihitaji.
Sasa suala hili ndilo lililoifanya serikali ya Taiwan mjini Taipei kuikosoa China kwamba inatumia chanjo kutafuta usuhuba wa kutafuta kukubalika.
Huko Uingereza nako waziri anayehusika na chanjo Nadhim Zahawi amesema wataanzisha mchakato wa kutoa chanjo haraka zaidi katika maeneo ambayo aina mpya ya kirusi kutoka India kimegunduliwa.
Shirika la afya ya umma la England PHE jana liliarifu kwamba jumla ya visa 1,313 vya maambukizi ya kirusi hicho vimethibitishwa kote Uingereza katika kipindi cha wiki moja iliyopita..