Japan na Marekani kuimarisha ushirikiano wa kiusalama
11 Aprili 2024Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida wametangaza mipango ya kuimarisha ushirikiano wa kiusalama baada ya kukutana siku ya Jumatano mjini Washington.
Mkutano huo wa pande mbili umefanyika wakati Marekani ikitafuta ushirika wenye nguvu zaidi wa Asia, huku China ikiongeza matumizi ya kijeshi na kujiimarisha zaidi katika mizozo ya kikanda katika Bahari ya China Kusini.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Biden amesema kwa mara ya kwanza, Japan, Marekani na Australia zitaunda mtandao wa pamoja wa ulinzi wa makombora ya anga. Nchi hizo tatu ni wanachama wa kundi linalofahamika kama Quad, linalojumuisha Marekani, Japan, Australia na India.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Kishida alisema Marekani na Japan zitaendelea kushughulikia changamoto zinazohusu China kupitia uratibu wa pamoja.