1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan yakabiliana na tetemeko la ardhi

12 Machi 2011

Raia wa Japan wanakabiliana na uharibifu uliotokea kwenye pwani ya kaskazini-mashariki. Moto ni mkali na maeneo katika baadhi ya miji yamefunikwa na maji baada ya kutokea tetemeko kubwa la ardhi na mawimbi ya Tsunami.

https://p.dw.com/p/10Xv8
Magari na vifusi vilivyosombwa na Tsunami JapanPicha: dapd

Tetemeko hilo la ardhi lenye kipimo cha 8.9 cha Richta ni kubwa kuwahi kutokea Japan tangu nchi hiyo ilipoanza kuweka kumbukumbu. Polisi wameripoti kupata miili ya watu 200 hadi 300 katika pwani.

Shirika la habari la Kyodo limesema idadi ya watu waliokufa inaweza ikafikia 1,000. Mawimbi ya mita 10 ya maji yalisafirisha meli zenye makontena, magari na kifusi katika mitaa ya mji wa Sendai na katika eneo la wazi la mashamba. Viongozi wamesema zaidi ya nyumba 3,000 zimeharibiwa au kuzolewa na maji.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Japan, Naoto Kan, leo ameongeza eneo la kuwaondoa watu karibu na kinu cha nyuklia cha Fukushima Daiichi hadi eneo la kilometa 10 huku kukiwa na uwezakano wa kutokea mionzi baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea jana.

Japan Erdbeben Tsunami Flash-Galerie
Kinu cha nyuklia cha Fukushima, JapanPicha: dapd

Jopo la usalama wa nyuklia limesema kuwa viwango vya mionzi vilikuwa mara 1,000 zaidi ya kiwango cha kawaida katika chumba cha udhibiti kwenye kinu hicho cha nyuklia, baada ya tetemeko hilo la ardhi kuharibu mfumo wa baridi.

Shirika la utangazaji la Japan-NHK, limewanukuu maafisa wa usalama wakisema kwamba hakuna madhara yoyote ya kiafya ambayo yametokea kwa wakaazi waliyoko karibu tangu kinu hicho kianze kuvuja na kwamba watu wametakiwa kuondoka katika eneo hilo kwa utulivu. Jumla ya watu 45,000 wametakiwa kuondoka. Jana watu 6,000 wanaoishi umbali wa kilometa tatu karibu na kinu hicho walitakiwa waondoke.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE,RTRE,DPAE)
Mhariri: Aboubakary Liongo