1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Kenya itaweza kukomesha kitisho cha UKIMWI ifikapo 2030?

2 Desemba 2024

Licha ya idadi ya wanaoishi na virusi kupungua kwa asilimia 3.3, watu 20,480 walifariki kutokana na athari ya maambukizi idadi iliyopanda.

https://p.dw.com/p/4negH
VVU Ukimwi | Mwathiriwa wa VVU akimeza dawa Nairobi Kenya
Kenya imefanikiwa kutimiza malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI ya asilimia 95 ya watu katika taifa kupata vipimo na kuhakikisha asilimia 95 ya wanaougua wako chini ya mpango wa dawa za kupunguza makali.Picha: Donwilson Odhiambo/ZUMA/picture alliance

Taifa la Kenya linaorodheshwa katika nafasi ya 7 duniani na la 6 barani Afrika nyuma ya Afrika Kusini, Mozambique, Tanzania, Nigeria na Zambia katika viwango vya juu vya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI takwimu zaidi zikionyesha kuwa, watu watatu kati ya wakenya 100 wana Virusi Vya UKIMWI. 

Kulingana na takwimu kutoka Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa (NSDCC) za mwaka 2023 jimbo la Kisumu linaongoza kwa idadi ya watu wanaoishi na virusi vya HIV. 

Taifa la Kenya linalenga kukomesha UKIMWI kama kitisho kwa umma ifikapo mwaka 2030, hii ikiwa ni sambamba na mpango wa Umoja wa Mataifa, hata hivyo, licha ya hatua zinazowekwa kufikia malengo haya, changamoto mbali mbali zinazidi kuibuka miongoni mwa mataifa yanayokua kiuchumi ikiwemo Kenya ambayo inakabiliwa na kitisho cha ufadhili katika harakati za upambanaji.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni kupunguzwa kwa bajeti za ufadhili wa hatua za upambanaji, hatua hii ikitajwa kuchangia kupunguza kasi ya uhamasishaji, harakati za kuwashirikisha mabalozi wa afya ya kijamii kuzuia mambukizi zaidi miongoni mwa akina mama wajawazito na watoto, upatikanaji wa huduma zinazofungamana na mipira ya kondomu, dawa za kupunguza makali miongoni mwa hatua nyingine muhimu.

Miongoni mwa kinga dhidi ya virusi vya ukimwi ni matumizi ya mipira ya kondomu wakati wa kujamiiana.
Miongoni mwa kinga dhidi ya virusi vya ukimwi ni matumizi ya mipira ya kondomu wakati wa kujamiiana.Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Global Fund: Mipango iliyobuniwa Kenya kupambana na UKIMWI imepiga hatua kubwa

Mwanachama na mwakilishi wa vijana wa shirika la Global Fund linaloratibu utaratibu wa Ufadhili wa kimataifa Mary Anne Wambugu, amesema mipango iliyobuniwa nchini kupambana na UKIMWI imepiga hatua kubwa, dawa za kufubaza makali maarufu ARVs zikitolewa bila malipo katika vituo vya afya ya umma na pia vya kidini yakiwemo na mashirika ambayo sio ya kiserikali, Shirika la Msalaba Mwekundu na AMREF. 

"Global Fund inapeana pesa miaka 3, yetu iliisha Juni mwezi huu lakini kuna awamu nyingine, ukweli ni pesa zimepungua kwa ukubwa ila pesa za matibabu bado ziko, kwa sababu tumewekwa katika kiwango cha juu kama nchi, haimaanishi tutaolewa mara moja, kumekuwa na mazungumzo vile pefa PEPSAR na Global Fund watatuacha," amesema Mary Anne.

Kupungua kwa bajeti kumeingilia mkwamo wa baadhi ya huduma, hasaa uhamasishaji serikali za kaunti zikikabiliwa na ugumu wa kuziba mwanya unaosababishwa na mapungufu ya bajeti, mfano kuondolewa kwa mipango ya kutoa chakula kama uji au nauli kwa wanaofika kupata dawa za kupunguza makali, mikusanyiko ya uhamasishaji, ushauri na kutiana moyo miongoni mwa mipango mingine.

Kando na mikwamo mbali mbali, mwaka huu Kenya imefanikiwa kutimiza malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI ya asilimia 95 ya watu katika taifa kupata vipimo, kuhakikisha asilimia 95 ya wanaougua wako chini ya mpango wa dawa za kupunguza makali na asilimia 95 ya wanaomeza dawa wamefaulu kuimarisha kinga ya mwili .

Mashindano ya urembo kupambana na unyanyapaa

"Ungepata watu wamepanga laini sahii hakuna mtu ana kuja anakaa na bado anatakiwa kumeza ARVs na nyumbani hakuna chakula, sahizi hakuna pesa za kuweka watu pamoja," amesema MaryAnne. 

Wito watolewa wa taifa la Kenya kutathmini upya harakati za kupambana na VVU

Hoja za kudumishwa ushirikiano zaidi miongoni mwa washikadau wote katika sekta ya afya wakiwemo wafadhili katika kupambana na makali ya UKIMWI zikitolewa, serikali kupitia wizara ya afya chini ya waziri Dkt. Deborah Barasa ameelezea hali ya kitaifa katika vyombo vya habari nchini akisema ni wakati kwa taifa kutathmini upya harakati za mapambano.  

"Wakati umefika tufanye mazungumzo ya wazi kuhusu kujitegemea na kubuni mipango endelevu ya HIV"

Watu milioni 1.3 wanaishi na virusi hivi, wanawake 890,747 na wanaume 487,710 tathmini ya ndani ya miaka 10 ikionyesha kupungua kwa maambukizi mapya kwa asilimia 83 kati ya mwaka 2013 - 2023, maambukizi  miongoni mwa watoto yamepungua kwa asilimia 71. 

Licha ya idadi ya wanaoishi na virusi kupungua kwa asilimia 3.3, watu 20,480 walifariki kutokana na athari ya maambukizi idadi iliyopanda na takriban watu 2,000 ikilinganishwa na mwaka 2022, jimbo la Kisumu likiongoza kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI Kwa asilimia 11.7.