1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, M23 imehusika na shughuli za uchimbaji madini?

Saleh Mwanamilongo
16 Mei 2024

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa wito wa kuzuiwa kimataifa kwa biashara ya madini kutoka nchi jirani ya Rwanda, ambayo Kongo inaituhumu kutumia vikundi vya waasi kuiba rasilimali zake.

https://p.dw.com/p/4fwrG
Waasi wa M23 walichukuwa udhibiti wa mji wa Rubaya wenye utajiri wa madini ya coltan, ambayo ni  muhimu katika utengenezaji wa simu za kisasa
Waasi wa M23 walichukuwa udhibiti wa mji wa Rubaya wenye utajiri wa madini ya coltan, ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa simu za kisasa Picha: DW/S. Schlindwein

Voltaire Batundi, kiongozi wa mashirika ya kiraia mtaani Masisi, jimboni Kivu Kaskazini, amesema waasi wa M23 wamehusika na uchimbaji madini ya Coltan huko Rubaya. Mji wa Rubaya una mabaki ya tantalum, ambayo hutolewa kutoka kwenye madini ya coltan, ambayo ni  muhimu katika utengenezaji wa simu za kisasa.

Batundi amesema bei ya kilogramu moja ya madini ya Coltan imepanda kutoka dola 30 hadi dola 70 toka kushikiliwa kwa mji huo na waasi wa M23.

''Waasi wa M23 wapo mjini Rubaya, wapo maeneo ya migodi. Walisambaza majembe kulikuwa na lori mbili ambazo zilikuja na majembe ili kuwapa watu wachimbe madini. Uchimbaji madini unaendelea sana Rubaya. Kuna ushahidi tosha kwamba walikuja kutafuta madini hayo.'', alisema Batundi. 

Hata hivyo, hakukuwa na duru zilizo huru kuthibitisha taarifa hii. Waziri wa Kongo wa madini , Antoinette N'Samba Kalambayi amesema serikali ya Kongo imepiga marufuku uchimbaji haramu wa madini, hasa hayo ya Coltan na Dhahabu huko Kivu ya Kaskazini. Waziri N'samba amezitaka nchi na mashirika ya kimataifa kuiwekea Rwanda vikwazo kuhusu kile alichokiita "madini ya damu" yanayosafirishwa kwa njia ya magendo na nchi hiyo.

M23 wakanusha tuhuma

Juhudi za DW kupata maoni ya serikali ya Rwanda, iliyoshutumiwa na Umoja wa Mataifa kuwaunga mkono waasi wa M23, hazikufua dafu.

Kwa upande wao waasi wa M23 walitupilia mbali tuhuma hizo na kusema hazina msingi wowote. Kundi hilo la waasi limeiambia DW kwamba kiongozi wao, Corneille Nangaa, tayari amepiga marufuku kwa wanachama na wapiganaji wa M23 kuyafikia maeneo ya uchimbaji madini yalioko chini ya udhibiti wao.

"Wanunuzi wa madini huko watalipa kodi kwa M23"

Udhibiti wa maeneo ya madini ndio chanzo cha machafuko ya mashariki mwa Kongo kwa zaidi ya miongo mitatu sasa
Udhibiti wa maeneo ya madini ndio chanzo cha machafuko ya mashariki mwa Kongo kwa zaidi ya miongo mitatu sasaPicha: Imago Images/photothek/M. Gottschalk

Reagan Miviri, mtafiti kuhusu Kongo katika taasisi ya Ebuteli,inayofadhiliwa na chuo kikuu cha NewYork, Marekani, amesema kwamba udhibiti mji wa Rubaya, wenye umuhimu mkubwa wa uchimbaji madini, utawaruhusu waasi hao wa M23 kutanua ushawishi wao.

''Tunaweza kusema kuwa huu ni mgodi wa kwanza ambao uko chini ya udhibiti wa waasi wa M23. Na ni wazi kwamba M23 watashiriki katika msururu wa usambazaji madini, kwa njia moja au nyingine, yenye umuhimu wa kimkakati. Hivi sasa wanunuzi wa madini huko watalipa kodi kwa M23, pia waasi hao watahakikisha madini hayo yanasafirishwa hadi ngome yao ya Bunagana kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.'', alisema Miviri. 

Mji wa Rubaya ni umbali wa kilomita arobaini kaskazini-magharibi mwa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini.

Shinikizo za kidiploamisia

Huku hayo yakijiri, afisa mkuu wa Marekani amesema nchi ya Angola inafanya kazi ya kuwaleta pamoja viongozi wa Rwanda na yule wa Kongo kutokana na kuongezeka kwa mvutano baada ya shambulio la Mei 3 kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani.

Molly Phee, mwanadiplomasia mkuu wa Marekani anayehusika na bara la Afrika, amekiambia kikao cha Bunge Jumatano kuwa Rais wa Angola Joao Lourenco anajaribu kuwaleta pamoja viongozi hao wawili ili kuzifanyia kazi hatua ambazo zimeamuliwa na Marekani na viongozi wa kikanda.

Phee amesema Marekani imedhamiria kuendelea na mikakati ya kujaribu kupunguza madhila huko mashariki mwa Kongo. Angola, ambayo ni mshirika wa Washington imekuwa pia ikiongoza harakati za kidiplomasia katika lengo la kumaliza miaka mingi ya ukosefu wa utulivu nchini Kongo.