1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Netanyahu kufutiwa kesi ya rushwa inayomkabili?

16 Januari 2022

Ikiwa makubaliano yatafikiwa na kusainiwa wiki ijayo huenda Netanyahu ataondoka kwenye jukwaa la siasa nchini Israel na mpambano wa kuwania uongozi wa Likud kuanza.

https://p.dw.com/p/45bKy
Israel Knesset | Netanjahu
Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Waziri mkuu wa zamani wa Israel Benjamin Netanyahu yuko kwenye mazungumzo ya kutafuta makubaliano katika ombi lake kwenye kesi ya rushwa inayomuandama ambapo inaelezwa kwamba makubaliano huenda yakatiwa saini mwanzoni mwa wiki.

Chanzo kinachohusika kwenye mazungumzo hayo kimebaini siku ya Jumapili kwamba inawezekana makubaliano hayo yakamfanya Netanyahu aondoke kwenye jukwaa la siasa za Israel kwa miaka kadhaa na kufungua kinyan'ganyiro cha kuwania uongozi wa chama chake cha  likud na kuutikisa mwelekeo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Makubaliano ya aina yoyote yatakayofikiwa yanaweza pia kumuepusha Netanyahu na kesi ya fedheha ya muda mrefu ambayo imelikumba taifa na kutishia kumharibia sifa yake baada ya uongozi. Hata hivyo msemaji wa Netanyahu amekataa kuzungumza chochote.

Israel Knesset | Netanjahu
Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Netanyahu anakabiliwa na kesi ya udanganyifu, kuvunja uaminifu pamoja na kupokea rushwa katika kesi tatu tofauti, ingawa waziri mkuu huyo wa zamani ambaye hivi sasa ni kiongozi wa upinzani, ameyapinga na kushikilia hana kosa.

Mtu anayehusika kwenye mazungumzo yanayoelezwa kuendelea ambaye jina linawekwa kapuni kwasababu hana mamlaka ya kuzungumzia undani wa mazungumzo hayo, amesema makubaliano kuhusu ombi lililotolewa yanaweza kutoa fursa ya kufutwa kwa kesi ya mashtaka ya rushwa na udanganyifu na kuifuta kabisa moja ya kesi zinazomkabili. 

Mtu huyo pia amesema kuna vipengele kadhaa bado havijatatuliwa ikiwemo kile kinachojumuisha kosa la ukosefu wa maadili ambalo chini ya sheria ya Israel linaweza kumfanya Netanyahu kuzuiwa kujihusisha na siasa kwa miaka saba. Aidha wanatafakari pia ikiwa Netanyahu atalazimika kutoa huduma za kijamii chini ya makubaliano hayo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri. Tatu Karema

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW