Je, Pakistan itawatimua wakimbizi mil. 1.7 wa Afghanistan?
5 Oktoba 2023Pakistan ilisema siku ya Jumanne kuwa raia milioni 1.73 wa Afghanistan wanaoishi nchini humo bila nyaraka za kisheria wana "tarehe ya mwisho ya Novemba 1" kuondoka kwa hiari, huku serikali ikidai kuwa raia wa Afghanistan walihusika na milipuko 14 ya kujitoa mhanga nchini Pakistan mwaka huu.
Serikali ya Pakistan ilisema wale wasioondoka kwa hiari watarudishwa kwa nguvu, ingawa haikuwa wazi namna watakavyowafuatilia wale walioondoka au kuwatafuta wale ambao hawakuondoka.
"Ikiwa hawatakwenda ... basi vyombo vyote vya usimamizi wa sheria katika majimbo au serikali ya shirikisho vitatumika kuwafukuza," Waziri wa Mambo ya Ndani wa muda Sarfraz Bugti aliwaambia waandishi wa habari mjini Islamabad.
Aliongeza kuwa serikali itataifisha mali za wahamiaji wasio na vibali, pamoja na kuweka njia ya kutoa taarifa kwa umma kuwashtaki watu wanaoshukiwa kuwa wahamiaji wa Afghanistan wasio na vibali. Hata hivyo, mchambuzi wa Pakistani Zahid Hussain aliiambia DW kuwa ana mashaka iwapo mamlaka zinaweza kutekeleza uhamishaji huo.
"Pakistani haitaweza kuwapata kwasababu wamesambaa kote nchini," alisema. Hussain aliongeza kuwa itakuwa vigumu kubainisha watu watakaofukuzwa kwani wengi wameishi Pakistan kwa muda mrefu na wameoa raia wa Pakistani.
Soma pia: Pakistan kuwafurusha wahamiaji mwezi ujao
"Wanaweza kupata baadhi, lakini kwa ujumla, ni vigumu kutofautisha," aliongeza. "Itakuwa vigumu kuwafuatilia kwani Islamabad imepitisha sera ya kuwaruhusu kwa kipindi cha miaka 40 wakati wa uwepo wa Marekani nchini Afghanistan, na ghafla mabadiliko haya ya sera hayatafanya kazi."
Ukandamizaji wa Pakistan dhidi ya wahamiaji wa Afghanistan
Hapo awali Pakistan iliwaweka kizuizini wakimbizi wa Afghanistan na kuwafukuza mara kwa mara kwa idadi ndogo.
Hata hivyo, uamuzi wa wiki hii wa kuwatimua Waafghanistan wasio na hati unawakilisha ongezeko kubwa. Hatua hiyo imekuja baada ya miezi kadhaa ya mvutano uliokithiri kati ya Afghanistan na Pakistan, ambao umesambaa na kuwa msako mkali dhidi ya wakimbizi wa Afghanistan.
Pamoja na mambo mengine, Pakistan inataka kuishinikiza serikali ya Taliban mjini Kabul kuzuia shughuli za mtandao wa wanamgambo wa Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP), unaoendesha shughuli zake katika maeneo ya mpaka wa Afghanistan na Pakistani na ambao umehusishwa na mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama vya Pakistan na milipuko ya kujitoa mhanga nchini Pakistan.
Qamar Cheema, mchambuzi wa masuala ya usalama nchini Pakistan, aliiambia DW kwamba serikali ya Pakistani ina wasiwasi kwamba TTP na kundi linalojiita "Dola la Kiislamu" (IS) wameajiri raia wa Afghanistan katika makundi yao.
"Shambulio kwenye mpaka wa Chitral na uvamizi wa hivi karibuni huko Balochistan hauwezekani bila msaada wa raia wa Afghanistan. Kundi la Taliban la Afghanistan linataka TTP iwe na hifadhi nchini Pakistan," Cheema alisema.
Soma pia: Idadi ya waliouwawa kwa bomu Pakistan yafikia 57
Mchambuzi huyo aliongeza kuwa mamlaka za Pakistani pia zinajaribu kuimarisha usalama kabla ya uchaguzi mkuu, ambao umepangwa kufanyika Januari 2024.
Hata hivyo, mashirika ya kiraia na mashirika ya wakimbizi yanasema kudai kuwa wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistan wanaunga mkono mashambulizi ya wanamgambo ni propaganda tu.
Kuwasili kwa wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistan pia kumesababisha wasiwasi mkubwa kwa wenyeji wengi. Wanaona ni kulemea uchumi wa nchi, kufyonza rasilimali zake za taifa na kubadilisha watu wa mikoa yao.
Wiki hii pia, Pakistan ilisema itahitaji pasipoti halali na visa kwa ajili ya kuingia kutoka Afghanistan, ikiachana na mazoea ya kutoa vibali maalum vya kusafiri kwa watu kutoka makabila yaliyogawanywa na mpaka.
Pakistan mpkeaji mkuu wa wakimbizi wa Afghanistan
Pakistan inasalia kuwa mojawapo ya nchi zinazohifadhi wakimbizi wengi zaidi duniani na imekumbwa na wimbi la wakimbizi wa Afghanistan. Hii imekuwa hivyo tangu uvamizi wa Kisoviet mwaka 1979 hadi utwaaji wa madaraka wa Taliban mwaka 2021, ambapo takriban wakimbizi 600,000 wa Afghanistan walikimbilia Pakistan.
Hata hivyo, idadi ya wahamiaji na wakimbizi inatofautiana kulingana na chanzo na inaweza kuwa vigumu kuthibitisha.
Shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, UNHCR, linakadiria jumla ya Waafghanistan milioni 3.7 wanaishi Pakistan. Zaidi ya milioni 1.3 ni wakimbizi wa Afghanistan waliosajiliwa. Wengine 840,000 wanashikilia "Kadi ya Uraia wa Afghanistan" (ACC). Inakadiriwa kuwa 775,000 hawana hati, na 600,000 ni wapya waliowasili tangu Agosti 2021.
Soma pia: Shambulizi la Bomu laangamiza maisha ya watu 52 Pakistan
Hali ya kisheria isiyoeleweka ya wahamiaji wengi wa Afghanistan, wakimbizi na wanaotafuta hifadhi nchini Pakistani kuhusu nyaraka pia inaonyeshwa na tofauti ya takwimu zinazotolewa na Umoja wa Mataifa na mamlaka ya Pakistani, ambao wanakadiria Waafghani milioni 4.4 wako Pakistan, kati yao milioni 1.7 "hawana hati. "
Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani Bugti anasema Waafghanistan ambao wamejiandikisha na mamlaka ya Pakistan hawahitaji kuogopa kufukuzwa, lakini inaweza kuwa haijulikani ni nani yuko katika kundi hili.
Kuingia na kuwepo kwa wakimbizi kunadhibitiwa chini ya Sheria ya Wageni ya Pakistani, ambayo inaipa mamlaka haki ya kuwakamata, kuwaweka kizuizini na kuwafukuza wageni, wakiwemo wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, ambao hawana nyaraka halali.
Wakati wakimbizi waliosajiliwa nchini Pakistani wanapewa ulinzi mdogo, Waafghanistan wasio na vibali wanakabiliwa na kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kufukuzwa nchini humo. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusitishwa kwa kuwarejesha kwa lazima raia wa Afghanistan.
Moniza Kakar, mwanasheria anayetoa msaada wa kisheria kwa wakimbizi wa Afghanistan mjini Karachi, alisema kumekuwa na mawimbi ya dhuluma dhidi ya wakimbizi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hasa baada ya uhusiano kuzorota kati ya Pakistan na Afghanistan.
"Kwa kawaida, wakimbizi wasio na viza au nyaraka za kisheria wanakabiliwa na kurudishwa Afghanistan, na baadhi ya familia hukimbilia kuhonga wasimamizi wa sheria," Kakar aliiambia DW.
Soma pia: Pakistan yafunga kivuko cha mpakani na Afghanistan
Pia alidai kuwa polisi wamewakamata raia wa Afghanistan ambao walikuwa wakiishi kihalali nchini Pakistan baada ya kuwanyang'anya usajili wao na kadi za uraia wa Afghanistan.
Wanaorudi wanakabiliwa na nini?
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, ni wakimbizi 8,000 pekee waliorejea Afghanistan mwaka 2023, asilimia 95 wakitokea Pakistan.
Farooq Khan, afisa wa zamani wa polisi wa Afghanistan kutoka mkoa wa Kandahar, alitafuta hifadhi Karachi wiki mbili kabla ya Taliban kuiteka Kabul mnamo Agosti 2021.
Ukandamizaji wa hivi karibuni nchini Pakistani umezua hofu kwake kutokana na visa yake iliyokwisha muda wake, na kumuacha akiishi kinyume cha sheria na hatari ya kufukuzwa nchini.
"Nimepunguza shughuli zangu za nje kutokana na hofu ya kukamatwa wakati wa msako unaoendelea," Khan aliiambia DW.
Alisema anahofia kurejeshwa kwa nguvu Afghanistan, ambako anaweza kufungwa jela au mbaya zaidi chini ya utawala wa Taliban kutokana na kujihusisha na serikali ya zamani.
Soma pia: Pakistan yaanza kuwazika wahanga zaidi ya 50 wa ugaidi
UNHCR inasema kwenye tovuti yake kwamba wakimbizi wanaorejea Afghanistan wanapata huduma za kimsingi za afya, malazi ya usiku inapohitajika na huduma nyinginezo.
"Kama sehemu ya msaada wake kwa wakimbizi wanaorejea nyumbani kwa hiari kutoka nchi walizopewa hifadhi. UNHCR inatoa kifurushi cha kuwarejesha makwao kwa hiari kinachojumuisha ruzuku ya pesa taslimu ya dola 375 kwa ajili ya kugharamia usafiri na mahitaji ya haraka wanapowasili."