Je, ukuwaji wa uchumi wa Afrika ni fumbo?
23 Mei 2013Bara la Afrika linasherehekea hivi sasa miaka 50 ya Umoja wa Afrika kwa ufanisi tangu wa kisiasa mpaka wa kiuchumi. Bara hilo linajitokeza kama eneo lenye fursa kubwa ya kuwavutia wawekezaji. Baada ya "Chui wa Asia" sasa Simba wa Afrika wananguruma.
Takwimu zinadhihirisha uchumi utakuwa mwaka huu kwa 7% au zaidi katika robo ya mataifa yote ya eneo la kusini mwa jangwa la Sahara. Wakati huo huo, mengi ya mataifa hayo yamo katika lile kundi la mataifa ambayo uchumi wake unakuwa haraka kupita kiasi.
Waafrika wawili kati ya watano wana simu ya mkononi au Smartphone. Nguvu za ununuzi zinazidi kukuwa barani Afrika na masoko yanaongezeka, huku matajiri wakizidi kuongezeka barani humo. Huu ni ufanisi wa kusisimua ambao watu wanapenda kuuzungumzia – naiwe wanasiasa, wanauchumi na pia vyombo vya habari.
“Afrika inajikwamua“, anasema mwandishi habari wa masuala ya kiuchumi Anver Versi. Mkenya huyo anaemiliki jarida la kiuchumi la African Business Magazine linalochapishwa mjini London anasema: "Kuna sababu nzuri za kuhoji kwamba Afrika itageuka kuwa soko muhimu la ukuaji wa kiuchumi katika miaka 50 inayokuja .Kwa sababu Afrika ina mali ghafi na nguvu kazi. Mtu anaweza kusema Afrika ni mahala pa kuvutia kabisa kuwekeza hivi sasa - Wachina wameitambua hali hiyo tangu miaka 10 au 15 iliyopita. Na sasa wajasiriamali wa Kijerumani na wazungu kwa jumla wanabidi wazindukane na kuitambua fursa hiyo."
Matumaini yana walakini
Kwa mujbu wa makadirio ya Benki Kuu ya Dunia, uchumi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara utakuwa kwa kadiri ya 5% katika kipindi cha mwaka 2013 na 2015. Uchumi wa dunia katika kipindi hicho hicho utakuwa kwa kadiri ya 3% tu.
“Viwango hivyo ni vya juu vya ukuaji wa kiuchumi, lakini hiyo bado si sababu ya kushangiria,“ anasema Robert Kappel. Mtaalam huyo wa Kijerumani anayeshughulikia masuala ya utafiti wa masuala ya Afrika katika taasisi ya GIGA mjini Hamburg, amechunguza makadirio ya ukuaji wa kiuchumi katika mataifa 42 ya kusini mwa jangwa la Sahara. Mengi ya mataifa hayo hayatofua dafu kwa mlinganisho wa kimataifa.
Robert Kappel anasema: "Ukuaji unatokana zaidi na ile hali kwamba mahitaji ya mali ghafi na bidhaa za mashambani yameongezeka sana katika kipindi cha miaka iliyopita na kwa namna hiyo bei nazo zimepanda. Kwa hivyo, inamaanisha biashara ya nje inachangia sana katika ukuaji wa kiuchumi barani Afrika na huo ni udhaifu mkubwa."
Taasisi kuu za fedha duniani, Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki Kuu ya Dunia, zote zinaonya juu ya bara la Afrika inategemea sana biashara na nchi za nje. Naye Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliyataka mataifa ya viwanda katika Kongamano la Kiuchumi la Kimataifa hivi karibuni mjini Cape Town nchini Afrika ya Kusini yawekwe sheria kali katika biashara ya mali ghafi pamoja na Afrika. “Rushwa na kukwepa kulipa kodi za mapato,“ anasema Kofi Annan, “ndio chanzo cha kudhoofika neema barani Afrika.“
Nini cha kufanya kuimarisha uchumi?
Shughuli za viwanda zinazorota barani Afrika na kilimo hakitoshi hata kukidhi mahitaji ya wakaazi wa bara hilo. Hata katika soko la ajira hakuna ishara ya kuongezeka nafasi za kazi. Hata katika nchi inayonyanyukia kiuchumi ya Afrika ya Kusini, zaidi ya 25% ya wakaazi wake hawana kazi na wanaoathirika zaidi ni vijana wanaoishi mashambani.
Kwa hivyo, nini cha kufanya ili ukuaji wa kiuchumi barani Afrika utuwame katika msingi imara? Mwandishi habari wa masuala ya kiuchumi, Anver Versi, anahisi panahitajika vitega uchumi zaidi katika miundo mbinu. Naye Robert Kappel wa Taasisi ya Uchunguzi wa Masuala ya Afrika anahisi mageuzi ya kiuchumi pia yanahitajika pamoja na sheria bora za uwekezaji ili kuwavutia wateja tangu wa ndani mpaka wa kimataifa.
Mwandishi: Julia Hahn/MMD Regionen Afrika
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Saumu Yusuf