Je, Uturuki ikaribishwe Umoja wa Ulaya ?
30 Machi 2010Maoni ya wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani,yamechambua zaidi mada mbili:ziara ya Kanzela Angela Merkel nchini Uturuki, na hodi-hodi za Uturuki, kujiunga na Umoja wa Ulaya.Mada ya pili, miripuko 2 ya wanawake 2 waliojiripua katika reli ya chini ya ardhi mjini Moscow:
Gazeti la Stuttgrater Nachrichten juu ya ziara ya Kanzela Merkel, nchini Uturuki, likiandika:
Tangu Bibi Merkel hata waziri mkuu Erdogan wa Uturuki,wanatupia zaidi macho sias.Na hii, yatupa kielezo kwanini, Kanzela Merkel muda mfupi kabla ya uchaguzi wa mkoa wa Mto Rhein amepalilia moto mada ya pendekezo la shule za waturuki nchini Ujerumani.Hatahivyo, wote 2 wanapaswa kuelewa wapi mikakati ya uchaguzi inamalizikia na wapi, dhara za muda mrefu katika usuhuba wao zinapoanzia.Imekawia lakini, pengine sio sana, Bibi Merkel na Bw, Erdogan wameonesha ni watu wenye dhamana kuelewa hayo."
Ama gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung laandika kwamba, katika diplomasia sio kiliomo bali kinachosemwa.Katika hali hii,bibi Angela Merkel amefaulu mengi mjini Ankara. Gazeti laongeza:
"Muhimu ni kuwa Uturuki, ikizidi kujitutumua kama dola la kimkoa, haitambi bila shabaha maalumu katika medani ya siasa za dunia.Kila Erdogan akiunyemelea uongozi wa Iran, kwa mfano, mara kwa mara amekuwa akiiumiza kichwa kambi ya magharibi.Lakini, katika usuhuba huo kuna pia fursa ya diplomasia kimataifa.Mchango wa Uturuki hapo kama mjenga daraja na Iran, umepigiwa upatu vya kutosha.Sasa lakini,wakati umewadia,kulitumia daraja hilo."
Gazeti la Oldenburgische Volkszeitung linaandika kwamba, bila ya shaka, Uturuki imepiga hatua kubwa katika njia yake ya kujiunga na Umoja wa Ulaya:Hatahivyo, laongeza gazeti:
"Uturuki iko mbali kabisa na kufunguliwa mlango kukaribishwa ndani ya UU....Kuwa Uturuki, imelikalia kijeshi eneo la kaskazini mwa Cyprus,ambalo tangu 2004 ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya,ni hali isiovumilika. Ufunguo muhimu wa kuleta ufumbuzi wa kukomesha kugawika kwa kisiwa cha Cyprus umo mikononi mwa Ankara."
Likitugeuzia mada, gazeti la Landeszeitung kutoka Lüneburg, likichambua mkasa wa jana wa kujiripua wanawake 2 mjini moscow na kuuwawa kwa watu kadhaa, laandika:
"Uongozi wa Urusi , utajibisha hujuma ya jana ya mabomu kwa mkono wa chuma.Kwani, ni sehemu ya fahamu ya warusi kuwa, ugaidi ujibiwe kwa nguvu kali.Katika kufanya hivyo, Moscow yaweza kutegemea msaada wa wa kambi ya magharibi.Kwani, kambi hiyo ikiongozwa na Marekani, kwa miaka mingi sasa, inatumia majeshi yake kupambana na ugaidi.Kurejea kwa ugaidi katika kitovu cha jiji la Moscow, kunachafua pia juhudi za mageuzi za rais Medwedew."
Gazeti la Sächsische Zeitung kutoka Dresden,likitukamilishia uchambuzi huu laandikaq:
"Uongozi wa Urusi, hautakubali kutishwa na vitendo vya kigaidi.Zaidi vitendo hivyo, vitawachochea rais Medwedew na waziri-mkuu Putin , kuzidi kupambana vikali na juhudi za kutaka kujitenga na Russia ......hatahivyo, ni kwa masilahi ya Urusi,sasa kusaka suluhisho la kisiasa la mgogoro wa miaka mingi sasa wa jimbo la Chechnia.Ikiwa haitafanikiwa hapo, eneo zima la Kaukasus laweza kufuka moto."
Mwandishi: Ramadhan Ali/DPA
Imepitiwa na Hamidou Oummilkheir