Kiongozi wa jeshi la Sudan akataa upatanisho na RSF
6 Januari 2024Burhan amesema ulimwengu mzima umeshuhudia namna waasi hao walivyofanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu huko Darfur Mashariki na kwingineko nchini Sudan.
Amewaambia wanajeshi waliokuwa wamekusanyika huko Port Sudan kwamba ni kwa sababu hiyo, hawatakubali kupatanishwa na wala hakutakuwa na makubaliano.
Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo amapema wiki hii alikubali kusitisha mapigano, kufuatia pendekezo la makundi ya kiraia, ingawa waangalizi walilionyesha wasiwasi kwa kuzingatia historia ya RSF ya kutotekeleza ahadi zake.
Hata kwenye mazungumzo yake na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, mjini Pretoria Daglo alisema yuko tayari kusitisha mapigano na kuvimaliza vita ambavyo vimeiharibu nchi yake.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano ya Sudan yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 12,000 huku wengine zaidi ya milioni 7 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.