Jeshi la Sudan laishutumu RSF kwa uhalifu wa kivita
15 Agosti 2023Burhan amesema hayo katika maadhimisho ya siku ya majeshi nchini humo, katikati ya mzozo kati yake na mshirika wake wa zamani anayeongoza vikosi vya dharura, Jenerali Hamdan Dagalo.
Kwenye hotuba yake ya nadra kupitia televisheni, Jenerali Abdel Fattah al Burhan amekishutumu kikosi hicho cha dharura, RSF na kiongozi wake Jenerali Hamdan Dagalo kwa ukiukaji, ikitumia kivuli cha ahadi za uongo za kurejesha demokrasia.
Amesema hayo wakati Sudan ikiadhimisha siku ya majeshi na kuongeza kuwa haiwezekani mtu mhalifu akarejesha demokrasia.
"Nchi yetu inakabiliwa na njama kubwa zaidi katika historia ya sasa, inayolenga utu, utambulisho, urithi na hatima ya watu wetu ambao tangu asubuhi ya Aprili 15, wamekabiliwa na uhalifu mbaya zaidi wa kivita na ugaidi, mikononi mwa wanamgambo wa muasi, msaliti Mohamed Hamdan Daglo na wasaidizi wake chini ya taasisi ya kilaghai inayoitwa Rapid Support Forces."
Sudan imetumbukia kwenye mzozo kufuatia mapigano yaliyochochewa na mvutano uliofukuta kwa miezi kadhaa kati ya Jenerali Abdel Fattah al Burhan wa vikosi vya Sudan na mpinzani wake, ambaye aliwahi kuwa msaidizi wake Jenerali Dagalo anayeongoza vikosi vya RSF. Mapigano hayo yameugubika mji mkuu Khartoum na kwingineko nchini humo, na tangu wakati huo pande hizo zinashutumiana kwa kuwaumiza raia na kukiuka makubaliano ya muda mfupi ya kusitisha vita.
Mapema mwezi huu, shirika la haki za binaadamu la kimataifa la Amnesty International lilizituhumu pande zote mbili kwa uhalifu mkubwa kabisa wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kukusudia ya raia na unyanyasaji wa kijinsia. Ripoti ya shirika hilo ilikilaumu kikosi cha RSF kwa kuhusika na karibu visa vyote vya ubakaji.
Katika hatua nyingine, mapigano yalishuhudiwa jana katika mji wa Khartoum na mji mkubwa wa jimbo la Darfur, hii ikiwa ni kulingana na mashuhuda, hatua iliyosababisha maelfu kuondoka.
Wakaazi wa eno hilo waliamshwa na milio ya risasi na makombora na siku ya Jumapili mamia waliyakimbia mashambulizi katika mji huo, wakati mapigano yakizidi kushika kasi katika siku za karibuni.
Huku hayo yakiendelea, shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF limeonya juu ya kitisho cha janga la kibinaadamu nchini Chad, katikati ya ongezeko la wakimbizi kutoka Sudan. Mratibu wa masuala ya dharura wa shirika hilo Susanna Borges amesema karibu wakimbizi 2,000 huingia Chad kila siku wakitokea Sudan.
Soma zaidi: OCHA: Watu milioni 3 wameyakimbia makaazi yao kutokana na vita nchini Sudan