1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jengo la ghorofa sita limeporomoka jijini Nairobi

Shisia Wasilwa6 Desemba 2019

Jengo lenye ghorofa sita limeporomoka jijini Nairobi Kenya, ambapo watu kadhaa wanahofiwa kufunikwa na vifusi vyake. Shughuli za uokozi zingali zinaendelea katika eneo la tukio hilo lililotokea mapema siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/3UKlk
Kenia | Mehrstöckiges Gebäude in Nairobi eingestürzt
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Senosi

Athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kote nchini Kenya zilibisha hodi katika mtaa wa Tassia, viungani mwa jiji la Nairoibi…Mvua hizo zilipopungua wakaazi waliamkia maafa na uharibifu wa makaazi yao.

Familia zaidi ya 40 zaathirika

Zaidi ya familia 40 zilizozukuwa zikiishi kwenye jengo hilo lenye ghorofa sita zikisalia bila makaazi. Shughuli za uokozi zinaendelea huku ikihofiwa kuwa watu kadhaa wameangamia kwa kufunikwa na vifusi. Jeshi la Ulinzi wa Taifa- KDF, linaongoza shughuli hizo. Afisa Mkuu wa Polisi katika jimbo la Nairobi, Phillip Ndolo amesema kwamba, "Nyumba 46 watu walikuwa wakikaa ndani, hatuwezi kujua ni watu wangapi wako humo ndani, tunaomba mtupe nafasi kwa sababu tuna vifaa vya kuwakoa wananchi hapo ndani.”

Kenia | Gebäudeeinsturz in Nairobi
Watu wakiendelea kuwatafuta watu wanahofiwa kufunikwa na kifusiPicha: DW/S. Wasilwa

Ripoti zinasema kuwa watu kadhaa wamepelekwa katika hospitali mbalimbali za Nairobi kwa matibabu. Polisi bado hawajatoa taarifa ya idadi ya watu waliofariki kwenye tukio hilo wala chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa zaidi ya familia 20 zilikuwa zimepangisha kwenye jengo hilo. Hata hivyo mwenye nyumba hizo hakuwepo wakati wa mkasa. Wakazi wanasema kuwa jengo hilo lilianza kutikisika kwenye msingi mapema asubuhi kabla ya kuporomoka. Purity Wanjiku amebahatika kunusurika na kadhia hii, kwani ilipotokea alikuwa ameelekea kazini, "tungependa serikali iangalie, maji kupita kwa milango sio vizuri, unyevuunyevu wa maji ndio umesababisha nyumba ianguke. Tunafaa kutengezewa mitaro, yenye maji yatakuwa yakipita.”

Huduma za dharura

Shirika la Msalaba Mwekundu limeweka kambi ya matibabu karibu na eneo hili ili kuwasaidia waathiriwa wa mkasa wenyewe. Tukio hili linajiri miezi michache tu baada ya wanafunzi saba wa shule ya msingi ya Talent Academy kuaga dunia na wengine 64 kujeruhiwa baada ya darasa lao kuporomoka. Mama Josphine aliponea tundu la sindano kwenye mkasa huo. Sasa anawatengezea chakula watu wanaohusika kwenye shughuli za uokozi. 

Kenia | Mehrstöckiges Gebäude in Nairobi eingestürzt
Wafanyakazi wa uokozi wakiendelea na zoezi la kuwatafuta watuPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Senosi

"Tumesikitika sana vile hii nyumba imeanguka. Ilianguka saa mbili na 47, tunasikitika magari ya kuokoa yalifika kuchelewa, na tungeokoa wenzetu wakiwa hai. Ninawasaidia na maji wapate nguvu ya kuwakoa wenzao," amesema mama Josphine.

Mwaka 2016, Mamlaka ya Ujenzi nchini Kenya ilitangaza kuwa asilimia 70 ya majengo yote yaliyoko jijini Nairobi hayakuwa salama kwa makaazi, hivyo ubomoaji wa majengo hayo ulianza, lakini ukasitishwa baada ya kipindi kifupi. Mkasa wenyewe unazikumbusha mamlaka dhima zao huku zikianikwa kwa kushindwa kumudu majukumu yao. Je, na kwa hili nalo, mamlaka husika zitarudi usingizini kabla ya kuamshwa na majanga mengine yajayo?