JERUSALEM: Olmert afanya ziara ya siku mbili nchini Uturuki
14 Februari 2007Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, anakwenda nchini Uturuki kwa ziara rasmi ya siku mbili. Ziara hiyo katika taifa hilo la kiislamu ambalo ni mshirika wa karibu wa Israel, inalenga kutafuta njia za kuutanzua mzozo baina ya Israel na Palestina na hofu kuhusu mpango wa Iran kutaka kumiliki silaha za kinyuklia.
Uturuki ambayo pia ni mshirika wa Marekani, imejitolea kusaidia katika juhudi za amani zinazofanywa na mataifa ya magharibi, kutumia uhusiano wake na Israel na Palestina na kuikaribia kwake Syria hivi majuzi.
Ziara ya waziri mkuu Ehud Olmert inafanyika siku chache kabla mkutano wa kilele wa siku tatu kati yake na rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Bi Condoleezza Rice. Wadadisi wameonya kwamba mkutano huo huenda usifaulu kuyafikia malengo yake.
Hapo kesho waziri Olmert amepangiwa kukutana na waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, waziri wa mambo ya kigeni, Abdullah Gul na maofisa wengine wa serikali kabla kurejea Israel.