Jeshi la AMISOM laongezewa muda Somalia
1 Novemba 2012Kurefushiwa muda kikosi cha AMISOM kunajiri wakati Baraza hilo lenye nchi wanachama 15 likijadili kuhusu ombi la Umoja wa Afrika la kutathmini kuhusu vikwazo vya silaha vilivyodumu miongo miwili dhidi ya nchi hiyo, ili kuisaidia serikali kupambana na wanamgambo wa kiislamu wenye msimamo mkali.
Wajumbe wa Umoja wa Mataifa walisema kuwa Baraza hilo bado limegawanyika kuhusu ombi la Umoja wa Afrika la kuanza kuruhusu uuzaji wa silaha kwa serikali ya Somalia. Pia limegawanyika kuhusu miito ya kuiruhusu Somalia kuuza nje makaa yaliyonaswa kutoka kwa wanamgambo wa al-Shabaab.
Baraza hilo la Usalama lilipiga kura kwa kauli moja kurefusha muda wa kuhudumu jeshi la kulinda amani Somalia - AMISOM, ambao ulitarajiwa kumalizika Jumatano (31.10.2012), hadi tarehe saba mwezi huu wa Novemba. Wajumbe wa baraza hilo wamesema watatayarisha azimio ifikapo Jumatano wiki ijayo ambalo litawezesha kuongezwa muda huo hadi mwaka mmoja.
Mazungumzo kuhusu Somalia kumalizika
Aidha walisema wiki ijayo watamaliza mazungumzo ya faraghani kuhusu Somalia ambayo yalivurugwa na kimbunga Sandy, ambacho kilisababisha ukosefu wa umeme na uharibifu mkubwa mjini Manhattan na kusababisha mafuriko katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa mto wa Mashariki ya jiji la New York.
Umoja wa Afrika umeliomba baraza hilo kutathmini upya vikwazo vya silaha dhidi ya Somalia ili kusaidia nchi hiyo kujenga upya jeshi lake na kuimarisha manufaa ya karibuni ya kijeshi dhidi ya kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Baraza hilo liliweka vikwazo hivyo mnamo mwaka wa 1992 ili kupunguza mtiririko wa silaha kwa wababe wa kivita, ambao mwaka mmoja baadaye walimuondoa madarakani kiongozi wa kiimla Mohamed Siad Bare na kuitumbukiza Somalia katika mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wajumbe katika mkutano huo walisema Kenya pia inaunga mkono kutolewa kibali cha kuuza hifadhi hizo za makaa katika mji wa bandari wa Somalia, Kismayu, ambao wanajeshi wa Kenya chini ya mwamvuli wa AMISOM waliutwaa mwishoni mwa mwezi uliopita, licha ya Umoja wa Mataifa kupiga marufuku uuzaji wa makaa. Kuna mgawanyiko kuhusiana na suala hilo huku baadhi ya nchi zikihofia kuwa wafanyabiashara wa Kismayu wanaofanya ushawishi kwa ajili ya uuzaji wa makaa hayo huenda wakawa na uhusiano na al-Shabaab.
Baraza hilo huenda likakumbwa na ugumu kukubali mauzo ya makaa hayo kutoka Somalia kwa sasa. Wajumbe wamesema Marekani ni mojawapo ya nchi ambazo zinaweza kukubali kuuzwa makaa hayo kama serikali ya Somalia itaidhinisha. Lakini serikali hiyo bado haijaunga mkono suala hilo. Baraza la Usalama lilipiga marufuku uuzaji makaa kutoka Somalia mwezi Februari mwaka huu katika jaribio la kusitisha ufadhili wa kundi la al-Shabaab.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo