Jeshi la Guinea laanza kujadili mustakabali wa taifa hilo
14 Septemba 2021Jeshi hilo leo linaanza mikutano ya siku nne kuhusu mustakabali wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi baada ya mapinduzi yaliyofanyika zaidi ya wiki moja iliyopita.
Wasiwasi unaongezeka kuhusu ni kwa namna gani jeshi hilo linaloongozwa na Mamady Doumbouya litaharakisha hatua ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia kama ilivyoagizwa na wasuluhisho wa jumuiya za kikanda na Kimataifa.
Mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yamepongezwa kwa tahadhari na wapinzani wengine wa muda mrefu wa rais aliyeondolewa Alpha Conde,akiwemo mpinzani maarufu Cello Dalein Diallo ambaye ameshindwa mara tatu na rais Conde katika chaguzi za rais nchini humo.
Katika mkutano wa leo Jeshi lililotwaa madaraka litakutana na maafisa kutoka chama cha Diallo cha Union of Democratic Forces of Guinea na wakosoaji wengine wa Conde.Baadae litafanya kikao na viongozi wa kidini.
Jana Jumatatu baada ya kukamilisha ziara yake mjini Conakry mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa katika ukanda wa nchi za Afrika Magharibi na Sahel Annadif Khatir Mahammat Saleh,alisema anaweka matumaini makubwa katika mikutano hiyo ya wiki hii.