Israel yazuia kombora la masafa marefu kutoka Yemen
15 Septemba 2024Kulingana na jeshi la Israel, kombora lililorushwa lilitua katika eneo la wazi na hakuna taarifa zozote za uwepo wa majeruhi waliotokana na shambulio hilo.
Tukio hilo lilisababisha kulia kwa ving'ora ikiwemo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Israel na katikati mwa Tel Aviv. Jeshi limeeleza kuwa, milio ya milipuko iliyosikika ilitokana na kuzuiwa na mfumo wa kujilinda dhidi ya makombora.
Itakumbukwa kuwa, jeshi la anga la Israel liliushambulia mji wa bandari wa Hodeidah nchini Yemen mnamo mwezi Julai na kusababisha vifo vya watu sita.
Soma zaidi: Wahouthi wa Yemen waapa kulipiza kisasi shambulizi la Israel Hodeida
Lilifanya shambulio hilo baada ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kuushambulia kwa droni mji wa Tel Aviv mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa upande wake afisa habari wa waasi hao kupitia ukurasa wake wa X amesema kombora la Yemen lilifika Israel baada ya majaribio 20 ya nchi hiyo kushindwa kulizuia.