Jeshi la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika litaanza shughuli zake Darfur mwanzo mwa mwakani
31 Oktoba 2007Sudan imeshikilia kwamba jeshi hilo karibu lote liwe kutoka nchi za Kiafrika.
Jeshi la askari 7,000 wa Umoja wa Afrika, AU, walioko sasa Darfur na ambao wameshindwa kuyakomesha michafuko katika sehemu hiyo ya mbali, Magharibi ya Sudan, litakuwa sehemu ya wanajeshi 26,000 wa Umoja wa Mataifa. Sudan sasa imekubali kuweko jeshi hilo kubwa la pamoja baada ya kuweko miezi ya mazungumzo, vitisho na mashauriano.
Rudolphe Adada, mkuu wa operesheni hiyo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, AU, aliwaambia waandishi wa habari huko el-Fasher ambako jeshi hilo litaanza kuendesha shughuli zake mwanzoni mwa mwakani. Alisema kikosi cha askari 4,000 wa Umoja wa Mataifa kitapelekwa huko kuongezea wanajeshi wa AU walioko ardhini. Lakini alisema bado wanangojea kupata kibali cha Sudan kuhusu ile orodha ya nchi zitakazochangia wanajeshi pamoja na masuala mengine yanayohusu usafiri kwa majeshi hayo, jambo ambalo Umoja wa Mataifa unataraji nchi za Magharibi zitatoa. Alisema wasiwasi pekee ni juu ya nchi moja au mbili hivi za Kiafrika ambazo zimeahidi kutoa baadhi ya wanajeshi wa nchi kavu, sababu ambayo imeifanya Sudan bado kutotoa kibali kuhusu mfumo wa jeshi zima. Sudan imeshikilia kwamba jeshi hilo karibu lote liwe na askari kutoka nchi za Kiafrika. Pendekezo la Umoja wa Mataifa ni kwamba asilimia 80 ya jeshi hilo litoke nchi za Kiafrika, asilimia 95 ya wanajeshi wa nchi kavu watokee Afrika.
Jeshi hilo, likipewa jina la UNAMID, mwanzo litakaa huko Darfur kwa miezi 12 na linatarajiwa kugharimu dola bilioni mbili kwa mwaka. Pia litafanya kazi chini ya uwezo wa ibara 7 ya Umoja wa Mataifa juu ya utumiaji nguvu. Jeshi hilo litaruhusiwa kutumia nguvu ili kujilinda na kuhakisha wafanya kazi wake na wale wa kutoa misaada wana uhuru wa kusafiri huko na kule. Nguvu pia zitatumiwa kuwalinda raia. Kamanda atakuwa Jenerali Martin Agwai wa kutokea Nigeria.
Ukosefu wa maji na kupatikana ardhi ya kujenga makaazi ya jeshi hilo ni kizuwizi kikubwa katika kupelekwa jeshi hilo, masuala ambayo lazima yatanzuliwe kikamilifu kabla ya jeshi hilo kuanza kuwalinda mamilioni ya watu wa Darfur wanaotegemea operesheni hiyo ya kutoa misaada.
Bwana Adada alisema ile tume ya kuangalia usitishaji wa mapigano uliofikiwa April 2004 itasitisha kazi zake kwa vile mazungumzo mepya yameanza katika mji wa Libya wa Sirte. Mkutano huo unatarajiwa kukubaliana juu ya mfumo wa mpito wa kuisimamia amri yeyote mpya ya kusitisha mapigano.
Lakini ilivyokuwa makundi muhimu ya waasi yanasusia mashauriano ya huko
Sirte, matarajio ya kupatikana amri ya mapema ya kusitisha mapigano yalitupiliwa mbali. Makundi hayo yametowa masharti magumu kuweza kuhudhuria na yameomba yapatiwe muda zaidi kuungana. Kiongozi muhimu wa waasi pia alisema yeye hatoshiriki katika mazungumzo hayo hadi pale Umoja wa Mataifa utakapokuweko Darfur kutoa ulinzi.
Wakati wapatanishi wa Umoja wa Mataifa na wa Umoja wa Afrika wamekataa kuyaahirisha mazungumzo hayo, licha ya kwamba waasi hawahudhurii, hata hivyo, watatuma kikundi kukutana na makundi ya waasi yanayokataa kwenda Sirte ili yafike kwenye meza ya mashauriano.