Jeshi la Russia laondoka Syria kwenda Libya?
19 Desemba 2024Wataalam wameeleza wasiwasi kwamba iwapo kambi hizo zitahamishiwa Libya, huenda hatua hiyo ikawa na athari kubwa kwa usalama katika ukanda wa Mediterrania, na hivyo kuzidisha hali ya mtikisiko wa kiusalama.
Je wanaondoka au hawaondoki Syria? Ndilo swali wachambuzi wa Mashariki ya Kati wamekuwa wakijiuliza katika siku kadhaa sasa.
Kwa kuangalia picha za satelaiti na kufuatilia matukio mitandaoni na angani, wachunguzi wa vyanzo huru, wamebaini matukio muhimu ya Urusi katika vituo vyake vya muda mrefu nchini Syria tangu utawala wa mshirika wake, dikteta wa Syria Bashar Assad, kupinduliwa takriban wiki mbili zilizopita.
Soma pia: HTS kujivunja na kujiunga na jeshi la Syria
Wachambuzi wanataja viashiria kama vile kuondolewa kwa vifaa vya kijeshi vya thamani kutoka Syria, kusimamishwa kwa mauzo ya ngano ya Urusi kwenda Syria ilhali katika miaka iliyopita, imekuwa msambazaji mkuu wa ngano kwa Syria, pamoja na hatua ya kundi la HTS kukataa msaada wa kibinadamu wa Urusi.
Pia wanasema popote ambapo meli za kijeshi za Urusi kutoka Tartus hatimaye zitaishia, itakuwa kiashiria muhimu cha wapi Urusi inaelekea, haswa ikiwa meli zitatia nanga kwenye bandari ya Tobruk ya Libya.
Kambi za Urusi nchini Syria zipo hatarini?
Wolfram Lacher, mshirika mkuu na mtaalamu wa matukio ndani ya Libya katika Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama, anasema kwa sasa hali haijawa bayana.
Soma pia: Mjumbe wa UN Syria ataka vikwazo viondolewe baada ya Assad
"Iwapo kambi za Syria zitazidi kuwa hatarishi kwa Urusi, basi umuhimu wa Libya utaongezeka. Inawezekana kwamba Urusi italazimika kuhamishia operesheni zake kutoka kambi za Syria kwenda Libya. Hata hivyo, hata kama hali bado haijathibitishwa wazi, tayari inaonekana kwamba Libya inapata umuhimu mkubwa zaidi kwa sababu kambi za Syria zinazidi kuwa hatarishi," amesema Lacher.
Soma pia: Baada ya Syria, je, utawala wa Iran utafuata na kuanguka?
Kulingana na Jalel Harchaoui, mwanasayansi wa siasa na mtaalamu wa Libya katika Taasisi ya Royal United Services ya Mafunzo ya Ulinzi na Usalama, (RUSI), nchini Uingereza, hivi sasa, hayo ni uvumi tu.
Harchaoui ameliambia DW kwamba iwe Warusi watasalia Syria au wataondoka, kuna ukweli fulani usiopingika ambao utabadilisha jinsi wanavyofanya kazi nchini Syria.
Ameongeza kuwa "hawataweza kuwa na kiwango sawa cha utulivu, usalama na uhakikisho kama hapo awali.”
Kwenda Libya?
Harchaoui amesema, "watakabiliwa na changamoto za kuhakikisha wanapata vifaa vyao muhimu, umeme, maji, na chakula. Aidha, wanatambua kuwa kuendesha kambi ya kijeshi katika nchi ya kigeni kunahitaji kuwa na ushirikiano mzuri na jamii inayowazunguka pamoja na msaada wa serikali, hasa katika masuala ya kiintelijensia."
Soma pia: EU kutuma mjumbe kuzungumza na viongozi wapya wa Syria
Wachambuzi wameripoti kuona mfumo wa ulinzi wa angani wa aina ya S-400 ukifunguliwa kwa ajili ya kusafirishwa, helikopta zikihamishwa, watu wakibeba masanduku ya usafiri wakiwa tayari kuondoka, na mizigo ikipakiwa kwenye ndege kubwa za kubeba mizigo zilizokuwa zimeegeshwa.
Aidha mnamo Disemba 11, manowari ya Urusi yaliondoka Syria, siku mbili kabla ya utawala wa Assad kuporomoka.
Lakini maafisa wa Urusi wamekanusha madai kwamba vikosi vyake vinaondoka Syria na imeripoti kwamba vinajadiliana na kundi la waasi lililoongoza mashambulizi yaliyouangusha utawala wa Assad na ambalo linaunda serikali ya mpito nchini humo.
Urusi ina kambi mbili muhimu za kijeshi nchini Syria. Kambi ya kijeshi ya majini Tartus iliyoanzishwa 1971 na kambi ya kijeshi ya angani iliyoko Hmeimim iliyoanzishwa mwaka 2015.