seehofer
12 Septemba 2013Wakati zimebakia siku kumi kufanyika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani watu katika jimbo la Bavaria ambalo ni kubwa kabisa nchini Ujerumani watapiga kura jumamosi ijayo. Uchaguzi huo unazingatiwa kuwa kipimo cha nguvu za vyama ndugu vinavyoiongoza serikali ya Ujerumani vya CDU, CSU na FDP.
Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer na chama chake yupo mbele ya chama kikuu cha upinzani SPD katika jimbo hilo. Kwa mujibu wa kura za maoni chama cha CSU kilichomo katika serikali ya mseto kinatarajiwa kufikia wingi wa uhakika wa zaidi ya asilimia 50.
Vyama vya CDU na CSU vimekuwa pamoja kama chanda na pete tokea mwaka wa 1949 na vimejenga ushirika wa wabunge bungeni .Kura za chama cha CSU ni muhimu kwa chama kikuu cha CDU katika chaguzi zote kuu za Ujerumani
Waliberali,FDP hawataki kushirikiana na wapinzani
Chama kingine ndugucha Waliberali,FDP leo kinatarajiwa kutamka wazi kwamba hakitakubali mseto na vyama vya upinzani vya SPD na Kijani, badala yake chama cha FDP kitasisitiza mfungamano na vyama ndugu vya CDU na CSU.
Wakati huo huo mgombea ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrück amemlaumu hasimu wake mkuu Kansela Merkel kwa kuficha ukweli juu ya mzigo unaobebwa na Wajerumani katika mgogoro wa madeni wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro.Akiyajibu maswali ya watu karibu 150 katika mji wa Mönchengladbach- magharibi mwa Ujerumani bwana Steinbrück alisema kuwa Kansela Merkel anawaficha Wajerumani ukweli juu ya mzigo wanaoubeba katika kuzisaidia nchi zenye madeni.
Bwana Steinbrück amesema Ujerumani inapaswa kuzisaidia nchi nyingine za ukanda wa sarafu ya Euro kwa kuuzingatia msingi wa mpango wa Marshal wa Marekani ulioisaida Ujerumani kujijenga upya baada ya vita kuu vya pili.Lakini amesemma badala yake Ujerumani imejiingiza katika Umoja wa kulipa madeni. Ametoa mfano juu ya hati za dhamana za Ugiriki.
Bwana Steinbrück ameeleza kwamba katika kila hati ya dhamana ya Ugiriki inayonunuliwa na Benki kuu ya Ulaya,ECB, Ujerumani inabeba dhamana ya asilimia 27. Bwana Steinbrück aliewahi kuwa waziri wa fedha wa Ujerumani ameweza kujiimarisha katika kura za maoni, siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi hapo tarehe 22 lakini bado yupo nyuma sana ya Kansela Merkel.Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU, vitafikia asilimia 39 ya kura wakati chama cha SPD kinatarajiwa kupata asilimia 25 ya kura.
Mwandishi:Mtullya Abdu/dpae, ZA.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman