Joe Biden amteua mwanamke kuwa mgombea mwenza
12 Agosti 2020Mgombea wa urais kupitia chama cha Democrat cha nchini Marekani Joe Biden amemteua seneta wa California Kamala Harris kuwa mgombea mwenza kwenye kinyang'anyiro hicho.
Hatua hiyo inaandika historia mpya nchini Marekani, katika wakati ambapo mwanamke huyo mweusi na raia wa kwanza mwenye asili mchanganyiko ya Marekani na Asia kugombea wadhifa wa juu katika kinyang'anyiro cha urais.
Harris aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter baada ya kuteuliwa akisema anajisikia heshima kuungana na Biden na amekubali kufanya kila liwezekanalo kumsaidia kuwa amiri jeshi mkuu.
Harris mwenye miaka 55, alikuwa karibu na mtoto wa kiume wa Biden Beau, aliyekuwa mwanasheria mkuu katika jimbo la Delaware, na yeye akiwa na wadhifa kama huo katika jimbo la California.
Biden kwenye ujumbe alioutuma kwenye mitandao yake ya kijamii ya alisema, "huko nyuma wakati Kamala akiwa mwanasheria mkuu, alifanya kazi karibu na Beau. Niliona namna walivyoshirikiana kuyashughulikia mabenki makubwa, kunyanyua mazingira ya wafanyakazi na kuwalinda wanawake na watoto kutoka kwenye unyanyasaji. Nilifurahia sana, na ninaona heshima sasa kuwa na yeye kama mwenzangu katika kampeni hii"