1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kufufua mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano

Oumilkheir Hamidou
21 Novemba 2017

Rais wa shirirkisho, Frank-Walter Steinmeier anaonana na viongozi wa FDP na die Grüne katika juhudi za kuyanusuru mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano baada ya mazungumzo hayo kuvunjika jumapili usiku.

https://p.dw.com/p/2o0Ll
Deutschland Schloss Bellevue Gespräch zu Koalitionsverhandlungen Die Grünen
Picha: picture-alliance/dpa/J. Denzel/Bundesregierung

Baadae leo rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier atakutana kwa mazungumzo katika kasri la Bellevue kwanza na viongozi wa chama cha walinzi wa mazingira die Grüne  Simone Peter na Cem Özdemir na baadae na mwenyekiti wa chama cha kiliberali cha FDP, Christian Lindner. Alkhamisi rais wa shirikisho atakutana na mwenyekiti wa chama cha Social Democrat, Martin Schulz.

Lengo la juhudi hizo ni kujaribu kuwatanabahisha viongozi hao umuhimu wa kuyanusuru mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano , baada ya mazungumzo hayo kuvunjika usiku wa manane wa jumapili kuamkia jumatatu ya jana. Hiyo hiyo jana rais wa shirikisho alikutana na kansela Angela Merkel na kuzungumzia baadae umuhimu kwa pande zote kutafakari misimamo yao na kuelezea shaka shaka zake kuelekea uchaguzi mpya.

Spoika wa bunge la shirikisho Wolfgang Schäuble
Spoika wa bunge la shirikisho Wolfgang SchäublePicha: Reuters/F. Bensch

Wolfgang Schäuble awahimiza wanasiasa waweke kando tofauti zao

Spika wa bunge la shirikisho, Wolfgang Schäuble, mtu wa pili mwenye usemi wenye nguvu humu nchini, akifungua kikako cha kwanza cha bunge mjini Berlin amewatolea wito wabunge na vyama vyao wasishikilie pekee miongozo ya wafuasi wao, bali watilie maanani pia kuundwa serikali iliyo imara.Jukumu hilo ni kubwa lakini linawezekana amesema spika wa bunge la shirikisho Wolfgang Schäuble na kuongeza tunanukuu:"Panahitajika moyo wa kuelewana katika jukumu kama hili gumu na tete, kwa vyama vyote vya kisiasa kuwajibika na kuweka kando kwa sehemu, ratiba za vyama vyao ili kuweza kufikia maridhiano ya kuunda serikali imara na ya walio wengi. Hilo si jambo la ajabu na wala halitodhoofisha msimamo wa yeyote yule."

Mkuu wa kundi la wabunge wa SPD katika bunge la shirikisho Bundestag
Mkuu wa kundi la wabunge wa SPD katika bunge la shirikisho BundestagPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

 SPD wanashikilia uchaguzi mpya uitishwe

Mkuu wa ofisi ya kansela Peter Altmeier nae pia amevitolea wito vyama vyote vya kisiasa viunge mkono juhudi za rais wa shirikisho."Kuundwa serikali kwa msingi wa matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita ni bora zaidi kuliko kampeni mpya za uchaguzi ambapo serikali itaundwa msimu wa kiangazi mwakani. Nae kiongozi wa kundi la SPD katika bunge la shirikisho, Andrea Nahles ametilia mkazo msimamo wa chama chake akisema hawatojiunga  kwa mara nyengine tena na serikali ya muungano wa vyama vikuu. Msimamo wa SPD unaungwa mkono na wafuiasi wake. Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa na gazeti la die Welt asili mia 18.2 tu ya wanachama wa SPD ndio wanaunga mkono fikra ya kuundwa serikali ya muungano pamoja na CDU/CSU. Asili mia 40.4 wanataka uchaguzi mpya.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu