Juhudi za Pakistan na India kutatua mzozo wao.
11 Desemba 2008Matifa hayo mawili jirani yenye uwezo mkubwa wa zana za kinuklia, yameimarisha juhudi za kushughulikia mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia, ingawa juhudi hizo zinapingwa vikali na makundi yenye itikadi kali.
Shambulizi hilo lililotekelezwa katika maeneo matatu zikiwmo Hoteli mbili za kitalii, lilitishia juhudi za amani kati ya mataifa hayo.
Hakikisho hilo limetokea siku ya jumanne wakati serikali ya India ilipowasilishwa kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa ombi la kutaka kupigwa marufuku kwa kundi la kigaidi la Jamaat-ud-Dawa,linaloendesha shughuli zake nchini Pakistani, kwa madai ya kulisaidia kundi la Lashkar-e-Toiba kutekeleza shambulizi hilo la Mumbai.
Mataifa haya mawili yameonekana kujizua na kujongeleana zaidi katika kubadilishana habari kuhusiana na makundi yaliyotekeleza shambulizi hilo mbali na na kujenga imani na ushirikiano katika kukabiliana na makundi hayo ya kigaidi.
Kamati ya usalama ya baraza la mawaziri nchini Pakistan tayari imekutana na kutoa hakikisho kwamba serikali hiyo iko tayari kushirikiana na India katika uchunguzi kuhusu shambulizi hilo mbali na kubuniwa kwa tume ya pamoja ya kushughulikia suala la ugaidi.
Serikali hiyo ya rais Asif Al-Zardari pia inasema kuwa kamwe haitakubali ardhi yake kutumiwa kama maficho ya makundi ya kigaidi.
Kwa kudhihirisha hilo waziri mkuu nchini Pakistan Yousuf Raza Gilani amethibitisha kukamatwa kwa watu kadhaa wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la Lakshar-eToiba, akiwemo makamanda wa ngazi za juu Zaki-Ur-Rehman Lakhvi na mwenzake Zarar Shah.
Hata hivyo wadadisi wanahoji kuwa huenda itakuwa vigumu kuyaangamiza makundi ya kigaidi kama lile la Lakshar ambayo sasa yanaonekana kukita mizizi kutoka na kwamba yamekuwa yakipata ufadhili kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu katika serikali zilizopita.
Kumekuwa na shinikizo kutoka kwa makundi mbali mbali nchini India kikiwemo chama cha Bharatiya Janatta kinachozingatia siasa za mrengo wa kulia, kwamba India inapasa kuiadhibu Pakistan kwa shambulizi hilo la Mumbai.
Lakini matokeo ya uchaguzi wa hivi punde nchini India yanaonyesha kinyume ya hayo, kwani raia wa India wanapinga vikali matumizi ya silaha dhidi ya Pakistan, licha ya chama hicho cha Bhqaratiyya Janata kutumia suala hilo kama jukwaa la kampeini yake.
Katika waraka uliochapishwa katika gazeti la New York Times nchini Marekani, rais wa Pakistan Asif Al Zardari amelitaja shambulizi la Mumbai kuwa halikuilenga serikali ya India pekee bali pia lilikusudiwa kuitikisa serikali yake changa na mpango wa amani kati ya mataifa hayo mawili.
Shirika kamati ya mpango wa amani baina ya nchi hizo mbili lililobuniwa mwaka wa 1999, linasema kuwa kwa kuzingatia hali ilivyo sasa na historia ya uhasama baina ya mataifa hayo mawili, ushirikiano ndilo njia pekee ya kupambana na ugaidi kupinga matumizi ya zana za kinuklia ili kuleta amani katika eneo zima la Asia Kusini.