Jukwaa la Davos mwaka 2017
16 Januari 2017Katibu mkuu mpya wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres naye ametangaza atahudhuria jukwaa hilo.Mashirika yote muhimu ya kimataifa pia nayo yatawakilishwa katika mkutano huo wa Davos. Lakini mara hii kansela wa Ujerumani ndie atakayekosekana katika jukwaa hilo.
Klaus Schwab hana makosa. Na hata jukwaa hilo la kiuchumi duniani linalofanyika mjini Davos lililoasisiwa mwaka 1971 halina kosa. Lawama pia haziwezi kuelekezwa katika ukosefu wa uwiano kiuchumi katika jamii nyingi , pia katika ongezeko la hofu kuhusiana na utandawazi, na pia kukwama kwa maendeleo, matokeo ya kuwapo kwa siasa kali za mrengo wa kulia katika kura ya maoni nchini Uingereza iliyosababisha nchi hiyo kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya yaani Brexit na uchaguzi wa rais nchini Marekani.
Kwa vyovyote vile iwavyo mtu angeweza kufahamu nukuu hiyo , ambayo Schwab aliitoa katika mkutano na waandishi habari wakati wa ufunguzi wa kikao cha 47 cha jukwaa hilo la kiuchumi mjini Davos. Aliyategemea baadhi ya maandishi yake ambayo aliyaandika binafsi miaka 20 iliyopita.
Aliandika wakati huo akionya juu ya kuongezeka kwa siasa kali za mrengo wa kulia na kutoa wito , kwamba utandawazi unapaswa kuwasaidia watu na sio tu kwa watu wachache. Hali hiyo inahitajika hata hii leo.
Utandawazi
"Kila jaribio , Schwab anasema , la changamoto zenye utata katika dunia hii zitakazotatuliwa kwa jibu rahisi , litashindwa bila shaka". "Hatupaswi pekee kuacha suluhisho lipatikane kwa njia ya misimamo mikali." Jukwaa lake la kiuchumi duniani analiona Schwab kuwa moja kwa moja ni mswada mbadala.
Kila mwaka wanakusanyika mjini Davos watu wengi wenye mawazo na mitizamo tofauti , wanasiasa , wafanyabaishara na wawekezaji , lakini pia wataalamu, asasi za kijamii na wanaharakati wa masuala ya kijamii. Na kwa hiyo jukwaa hilo la kiuchumi linakuwa ni mkusanyiko wa kila mwaka wa viongozi wa juu duniani katika masuala mbali mbali.
Hapa wanakutana wanasiasa wenye madaraka makubwa duniani na watu wanaohusika na masuala ya kifedha. Na hapa pia kila mwaka kunahubiriwa , kuhusu utandawazi zaidi, kufungua mipaka ya biashara na kuondoa vizuwizi vya uwekezaji wa soko la hisa ili kuiweka dunia katika mahali bora zaidi. Bila shaka hali ya zamani ya uhakika inaonekana zaidi na zaidi kuwa inapotea.
Katika mataifa ya magharibi watu tayari wanajiuliza , iwapo utandawazi pamoja na ushindano wa kimataifa kama umeleta mafanikio yoyote. Katika kura ya kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya hilo lilichukua katika nafasi ya juu, na katika kuchaguliwa kwa Donald Trump halikadhalika. Schwab anatoa wito wa kuwa na mshikamano na uwiano. "Kila uchumi wa masoko anapatikana mshindi na mshindwa", anasema Schwab.
Kansela hatahudhuria
"Kusimama imara ndio pekee mfumo , ambao mshindi na mshindwa watakuwa na mshikamano." Kauli mbiu katika mkutano wa mwaka huu inasema, "Uongozi wenye uwajibikaji na unaoweza kubadilika kutokana na mahitaji". Ni dokezo kuhusu mtengano unaoongezeka baina ya sehemu kubwa ya wananchi na viongozi wa juu, na kukosekana hali ya kuziamini taasisi mbali mbali.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza kutohudhuria jukwaa hilo , kutokana na sababu za mipango ya matukio mengine ya kikazi. Badala yake waziri wa fedha Wolfgang Schaeuble na waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen watakwenda mjini Davos. Rais wa Ufaransa Francois Hollande atabakia nyumbani, waziri mkuu mpya wa Italia Paolo Gentiloni halikadhalika.
Lakini waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atakuwapo , hataka kama hakuna mipango kamili kwa ajili ya Brexit ambayo inatarajiwa. Wanasiasa muhimu kutoka Marekani hawatakuwapo mwaka huu, kwa kuwa Donald Trump ataapishwa tarehe 20 Januari ambayo ndio siku ya mwisho ya kongamano hilo.
Ni meneja wa zamani tu wa mifuko ya uwekezaji mbadala Anthony Scaramucci anatarajiwa , ambaye ndie aliyetayarisha sehemu ya timu ya Trump ya kipindi cha mpito inayomtayarishia hatua za kuingia madarakani.
Mwandishi : Andreas Becker / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Iddi Ssessanga