1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jukwaa la Kiuchumi la mjini Davos:

26 Januari 2004
https://p.dw.com/p/CHit
Mkutano wa kila mwaka unaojulikana kama Jukwaa la Kiuchumi Duniani, umemalizika jana katika kijiji cha Uswisi cha Davos, huku uchunguzi wa kura za maoni ukionyesha kwamba asili mia 60 ya walioshiriki wanaamini kwamba biashara ya mazao ya kilimo ndiyo suala muhimu la kuweza kuyafufua mazungumzo yaliokwama ya kile kinachojulikana kama Duru ya maendeleo ya Doha, chini ya Shirika la biashara duniani -WTO.
Wengi miongoni mwa wajumbe wapatao 2,000 , walioshiriki katika mkusanyiko huo wa davos wakiwemo wakuu wa makampuni ya kibiashara, maafisa wa shughuli za fedha , Viongozi wa serikali na wanauchumi, wana maoni ya kwamba kushindwa kwa mazungumzo ya biashara yanaweza kuiuwa kabisa duru ya Doha, ilioasisiwa na mawaziri wa biashara.
Mbali na suala hilo la kilimo, zingatio la walioshiriki katika mkutano huo,lilikua ni katika masuala kama kuanguka kwa thamani ya sarafu ya Dola na matokeo yake ambayo miongoni mwa mengine ni kupungua kwa kiwango cha bidhaa zinazoagizwa kutoka Umoja wa ulaya na japan na pia kupanda kwa thamani ya sarafu ya Euro na Yen ya Japan.

Halikadhalika washiriki walisema wana wasi wasi juu ya kufufuka kwa hali ya uchumi wa dunia, kukiongozwa na Marekani , China na India na iwapo mwenendo wa sasa utasababisha kuimarika kwa hali jumla ya kiuchumi duniani.
Kama kawaida tangu lilipoasisiwa jukwaa hili la Davos miaka 32 iliopita, kulikua pia na mikutano ya faragha miongoni mwa Wakuu wa makampuni ya biashara na Viongozi wa serikali kuhusiana na vitega uchumi.

Ama zingatio kubwa upande wa biashara lilikua ni kilimo. Rais wa Shirikisho la Uswisi Joseph Deiss, aliitisha mkutano wa mawaziri na maafisa wa ngazi ya juu wa biashara kutoka nchi 20-wanachama wa Shirika la biashara duniani, WTO- kuzungumzia hatima ya mazungumzo yaliokwama ambapo suala tete ni utaratibu unaotumiwa na Marekani na nchi za Ulaya kufidia wakulima wao-jambo ambalo linaangaliwa na nchi zinazoendelea kuwa ni mbinu ya kujilinda kibiashara na kuzifungia milango bidhaa za nchi changa kuingia katika masoko yao. Sera hizo zinatumika karibu katika mataifa yote ya viwanda. Kwa mujibu wa makadiro ya Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo barani Ulaya-likiwa kundi la mataifa tajiri ni kwamba wanachama wake hutumia jumla ya dola 320 bilioni kwa kufidia wakulima wao.

Itakumbukwa kwamba mkutano wa tano wa mawaziri wa Shirika hilo uliofanyika mwezi Septemba mwaka jana huko Cancun-Mexico ulishindwa kufikia makubaliano yoyote. Mawaziri wanchi 147 wanachama , walipaswa kufikia makubaliano katika mkutano huo juu ya ajenda iliokubaliwa mjini Doha, ambapo suala kuu ni hilo la kilimo.
Duru hiyo ya mazungumzo imepewa muda iwe imekamilishwa ifikapo Januari 1, 2005. Mkurugenzi mkuu wa WTO Supachai PANITCHPAKDI ambaye ni Waziri mkuu wa zamani wa Thailand anaendesha juhudi kabambe wakati huu, kuzishinikiza nchi wanachama ziwajibike ipasavyo .

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema Jumuiya za kiraia zina mchango muhimu wa kutoa kusaidia kuyaffufua mazungumzo ya Doha, ili kufungua njia ya kushajiisha maendeleo kwa mataifa ya kusini. Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa lisilokua la Kiserikali -Global Vision International- Dean .R. Hirsch, alisema kwa kuachwa tabia ya kujilinda kibiashara, nchi zinazohusika zitakua zimetoa mchango mkubwa wa kupunguza umasikini duniani, ambao unawaathiri karibu watu bilioni tatu.
Mbali na masuala ya kiuchumi mkutano wa Davos uligubikwa pia na maasuala ya kisiasa-kubwa zaidi likiwa ni vita vya Irak. Hata hivyo safari hii hakukua na maandamano makubwa ya wapinzani kama ilivyo kawaida ya mkutano huo wa Davos. Kundi dogo la waandamaji lilionekana siku hapo jumamosi kwenye stesheni kuu ya treni ya kijiji hicho. Pamoja na hayo polisi walikua katika ulinzi mkali wakati wote wa mkusanyiko huo wa siku tano,tayari kukabiliana na hali yoyote ya purukushani na vurugu.