1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Burundi kujadiliwa Dar es Salaam

6 Julai 2015

Mzozo ukiendelea nchini Burundi kuhusiana na azma ya rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula watatu, viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana jijini Da es Salaam leo kuujadili mzozo huwo.

https://p.dw.com/p/1FtLE
Burundi Imbonerakure Miliz
Picha: Getty Images/AFP/C. de Souza

Leo viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa kilele wa kuujadili mzozo unaoendelea Burundi. Huu ukiwa ni mkutano wa tatu kufanyika tangu kuanza kwa machafuko nchinihumo mwezi Aprili.

Hata hivyo msemaji mkuu wa rais wa Burundi Gervais Abahiro amesema, rais Pierre Nkurunziza hatoshiriki katika mkutano huo. Badala yake waziri wa mambo ya nchi za nje Alain Aime Nyamitwe, ndie anaeiwakilisha nchi hiyo. Rais huyo amebaki Burundi na anaendelea na kampeni zake za uchaguzi wa urais, unaotarajiwa kufanyika Julai 15. Uchaguzi ambao umezua machafuko makali miongoni mwa wananchi, wanaompinga rais huyo kugombea muhula wa tatu madarakani.

Mkutano huwo wa kilele unahudhuriwa na viongozi kutoka Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Hata hivyo Rais wa Rwanda Paul Kagame ambae alimtolea wito wa kujiuzuli rais Nkurunziza hahuhudhurii pia.

Jaribio la mapinduzi

Mwezi mei Nkurunziza alikabiliana na jaribio la mapinduzi wakati alipokuwa akihudhuria mkutano mwengine wa awali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioitishwa ili kujadili mzozo wa Burundi.

Wakati huohuo generali Leonard Ngendakumana ambae alishiriki katika jaribio hilo la mapinduzi ameapa kuendelea na mashambulizi dhidi ya rais huyo hadi pale serikali yake itakapoangushwa.

nach Putschversuch - Präsident Pierre Nkurunziza zurück im Amt
Rais wa Burundi Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

"Baada ya kushindwa kumpinduwa Nkurunziza Mei 15, bado lazima tuendele kupambana ili kumshinikiza kutafakari anachofanya na kujiuzulu," amesema Leonard Ngendakumana akizungumza na televisheni ya Kenya ya KTN.

Licha ya uchaguzi huwo kupingwa vikali, nchi hiyo ilifanya uchaguzi wa bunge Jumatatu iliyopita. Uchaguzi ambao ulisusiwa na vyama vya upinzani. Ujumbe wa usimamizi wa uchaguzi wa Umoja wa Mataifa umesema uchaguzi huwo ulifanyika katika hali ya utatanishi na katika mazingira ya hofu na vitisho. Matokeo bado hayajatangazwa.

Mpatanishi lazima ajiuzulu

Machafuko yakiwa yanaendelea nchini humo serikali ya chama tawala cha CNDD-FDD na washirika wake, wameuambia Umoja wa Mataifa kuwa mpatanishi wa mzozo wa Burundi Abdoulaye Bathily lazima ajiuzulu, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya kuchukua wadhifa huwo.

Msemaji mkuu wa chama hicho Gelase Daniel Ndabirabe amesema, chama chake kinamtaka ajiuzulu kwa kuwa mpatanishi huyo anashindwa kuheshimu uhuru wa Burundi.

Bathily alichukuwa nafasi ya mpatanishi wa zamani Said Djinnit, ambae alijiuzulu kufuati madai ya wapinzani kuwa anaelemea zaidi upande wa serikali.

Tangu kuanza kwa machafuko hayo nchini Burundi miezi miwili iliyopita, zaidi ya watu 70 wameuwawa. Na wengine 144,000 wamekimbilia nchi jirani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Iddi Ssessanga