1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juncker ashinikiza makubaliano na Ugiriki

13 Machi 2015

Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras wametowa wito wa mshikamano na Ugiriki kuinusuru isifilisike na kuhatarisha kutolewa katika kanda ya sarafu ya euro

https://p.dw.com/p/1EqVo
Mkuuu wa Hlamshauri ya Umoja wa Ulaya Jean Calude Juncker (kulia) na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras mjini Brussles. (13.03.2015)
Mkuuu wa Hlamshauri ya Umoja wa Ulaya Jean Calude Juncker (kulia) na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras mjini Brussles. (13.03.2015)Picha: Reuters/Y. Herman

Matamshi ya viongozi hao yanakuja wakati Ujerumani mfadhili mkuu wa Umoja wa Ulaya ikiishinikiza serikali mpya ya Ugiriki yenye sera kali za mrengo wa kushoto iheshimu ahadi zake ilizotowa kwa taasisi za mikopo za kimataifa na pia yanaonyesha wasi wasi wa Juncker juu ya hatari kwa Umoja wa Ulaya kupata madhara makubwa kutokana na mzozo huo na yumkini yakachochea tuhuma kutoka Ujerumani kwamba Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inaweza ikajaribu kupunguza makali ya makubaliano yoyote yale yatakayofikiwa.

Siku moja baada ya waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schauble kutamka hadharani kwamba Ugiriki yumkini ikatoka kweye kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya kwa sababu viongozi wake wameshindwa kufikia maafikiano juu ya mikopo mpya, Juncker ametowa kauli ya tahadhari kwa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Amewaambia waandishi wa habari Ijumaa (13.03.2015) wakati akimkaribisha Tsipras katika Halmashauri ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwamba hakuridhishwa na maendeleo yaliofikiwa katika mazungumzo ya hivi karibuni.

Juncker amekaririwa akisema "Nitatowa mapendekezo kadhaa kwa rafiki yangu Alexis na halafu tutaangalia hali itakavyokuwa.Nafuta kabisa uwezekano wa kushindwa na sitaki tushidwe.Huu sio wakati wa kutengana kwa watu wa Ulaya ni wakati wa kuungana."

Juncker ambaye kwa muda mrefu alikuwa waziri mkuu wa Luxembourg na kushika wadhifa wa kuwa kiongozi wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya hapo mwezi wa Novemba anahofia kwamba baadhi ya viongozi yumkini wakawa wanayakadiria vibaya madhara ya yatakayosababishwa na Ugiriki kutoka Umoja wa Ulaya.

Uwezekano kwa Ugiriki kutoka kanda ya euro

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Schauble amekiambia kituo cha utangazaji cha Austria hapo jana kwamba kuna hatari kwa Ugiriki kupoteza wanachama wake katika kanda ya sarafu ya euro barani Ulaya iwapo mazungumzo hayo yatashindwa kufanikiwa.

Wolfgang Schäuble waziri wa fedha wa Ujerumani.
Wolfgang Schäuble waziri wa fedha wa Ujerumani.Picha: Reuters/H. Hanschke

Amesema haondowi uwezekano huo kutokana na kwamba wajibu na uwezekano wa kutokea hilo uko mikononi mwa Wagiriki wenyewe na kwamba hawajuwi hasa kile wanachofanya viongozi hao wa Ugiriki.

Uchunguzi wa maoni umegunduwa kwamba zaidi ya nusu ya Wajerumani wanafikiri Ugiriki inapaswa kutoka kwenye kanda ya sarafu ya euro.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni Kansela Angela Merkel na waziri wake wa fedha Wolfgang Schauble wanaendelea kuwa wanasiasa mashuhuri kabisa nchini Ujerumani tafauti na vile wanavyochukiwa nchini Ugiriki kutokana na msimamo wao kushupalia nchi hiyo itekeleze hatua za kubana matumizi na mageuzi ili iweze kupatiwa mkopo wa kuizuwiya isifilisike na madeni.

Taasisi za mikopo zimekuwa zikidai nchi hiyo ifanye mageuzi kadhaa ya kiuchumi ili ipatiwe msaada wa mkopo uliobakia wa euro bilioni 7.2.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa/AP

Mhariri: Gakuba Daniel