Juncker atakiwa kuleta mabadiliko
23 Oktoba 2014Gazeti la "Braunschweiger Zeitung" linaandika: Mwenyekiti wa Kamisheni Jean-Claude Juncker ana majukumu mawili makubwa. Kwanza ni kupunguza mgawanyiko kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na raia wa kawaida. Wananchi lazima wawe na imani na Umoja huo. Na jukumu la pili ni kuuinua uchumi. Juncker ameahidi kuwa Umoja wake utawekeza Euro bilioni 300. Kwa tamko hilo ametoa ishara sahihi.
Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaeleza kuwa Umoja wa Ulaya uliundwa kama jaribio. Ni jaribio linaloelekea kuwa na mafanikio. Lakini sasa zipo changamoto kubwa zinazoikabili jumuiya hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anazitaja changamoto kuwa mgogoro wa kiuchumi, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na tatizo la wakimbizi. Anaendelea kusema "Umoja wa Ulaya lazima uanze kushughulikia matatizo hayo mara moja."
Wasichana wanataka mshikamano
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia pia vijana kutoka nchi za Magharibi wanaokwenda Syria na Iraq kujiunga na kundi linalojiita Dola la Kiislamu. Utakumbuka kuwa wiki hii wasichana watatu walikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Frankfurt hapa Ujerumani, wakiwa wanajaribu kusafiri kwenda Syria. Gazeti la "Eisenacher Presse" linaandika: "Lazima tujiulize kwanini idadi ya wasichana wanaojiunga na kundi la IS inaongezeka siku hadi siku. Inaelekea kwamba kundi hilo linawapa mshikamano ambao hawakupata kwenye familia zao au kutoka kwa jamii. Labda ujumbe wanaousambaza IS kupitia vyombo vya habari unawagusa zaidi wasichana hao kuliko ujumbe kutoka kwa wazazi wao ambao mara nyingi hawako tayari kuyasikiliza matatizo ya watoto wao."
Mhariri wa "Märkishe Allgemeine" anaziasa nchi za Magharibi zikubali kwamba vita dhidi ya Dola la Kiislamu si changamoto ya kijeshi tu. IS kupitia mkakati wake wa kusambaza video mtandaoni, imefanikiwa kuwafanya vijana waone kama vile mauaji ya kinyama yanayofanywa na kundi hilo ni kama jambo la kifahari, anasema mhariri huyo. Wanasiasa lazima waongeze juhudi zao kwani vijana wanaopigana wakirudi kwenye nchi zao wanakuwa tishio la usalama. Na ikibidi, serikali zinatakiwa pia kujaribu kuwafikia vijana kupitia mitandao kama vile Youtube na kadhalika.
Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Saumu Yusuf