Kabila aidhinishe harakati dhidi ya FDLR
9 Januari 2015Baraza hilo lenye nchi 15 wanachama limetishia kuwawekea vikwazo wafuasi wa kundi la FDLR, ambao wamepuuzilia mbali tarehe ya mwisho waliyowekewa kujisalimisha Januari 2 mwaka huu.
Mwito huo wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa umekuja siku moja baada ya katibu mkuu wa umoja huo Ban Ki Moon kuzungumza kwa njia ya simu na rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila na kumhimiza apitishe uamuzi dhidi ya waasi wa kundi la ukombozi wa Rwanda, FDLR. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, kinajiandaa kwa harati za kijeshi kuwachakaza na kuwaondoa kabisa waasi wa kundi hilo, lakini ufanisi wa tume hiyo unategemea ushiriki wa jeshi la serikali ya Kongo.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema serikali ya rais Kabila lazima iwe tayari mara tu harakati hiyo itakapoanza, na itume wanajeshi na maafisa wa polisi kulilinda eneo la mashariki mwa nchi kuwazuia waasi wa FDLR kurejea na kulidhibiti tena.
Umoja wa Mataifa unashinikiza makundi kadhaa ya waasi yapokonywe silaha baada ya miongo miwili ya vita na machafuko mashariki mwa Kongo, ambayo mengi yalichochewa na biashara ya madini yenye faida kubwa. Rais wa baraza la usalama na balozi wa Chile katika Umoja wa Mataifa, Cristian Barros Melet, amesema, "Baraza la usalama linasisitiza wasiwasi wake mkubwa kuhusu usalama na hali mbaya ya kibinadamu mashariki mwa Kongo kutokana na vitendo vya makundi ya waasi wenye silaha na linasisitiza umuhimu wa kuyaangamiza kabisa makundi yote likiwemo kundi la waasi wa Rwanda, FDLR."
Kundi la FDLR liangamizwe
Baada ya kuacha kuliunga mkongo kundi la waasi la M23 mwaka uliopita, Rwanda imetaka kundi la FDLR lipokonywe silaha, ambalo baadhi ya wanachama wake walihusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mnamo mwaka 1994, kabla kuvuka mpaka na kuingia Kongo.
Katika taarifa yake ya pamoja baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limesema operesheni dhidi ya FDLR lazima ianze mara moja. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema, "Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na serikali za kanda hiyo lazima sasa zitimize ahadi na wajibu wao kuchukua hatua ya haraka kuwapokonya silaha waasi wa FDLR." Power aidha amesema miaka 20 baada ya mauaji ya Rwanda hakutakiwi kuwa na masharti au kuchelewa katika kuifikisha kikomo historia ya kikatili ya kundi hilo na tabia yao ya kufanya uasi bila kuwa na hofu ya kushtakiwa.
Viongozi wa Kiafrika wanajiandaa kuijadili operesheni hiyo dhidi ya waasi wa kundi la FDLR katika mkutano wa kilele uliopangwa kufanyika mjini Luanda nchini Angola siku ya Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo. Afisa mmoja wa Marekani amesisitiza kwamba rais Kabila na viongozi wa mataifa ya Afrika wanatarajiwa kutimza ahadi zao na kuiunga mkono harakati ya kijeshi dhidi ya waasi hao.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/REUTERS
Mhariri: Iddi Ismael Sessanga