Kada wa upinzani apatikana na majeraha baada ya 'kutekwa'
2 Desemba 2024Chama cha upinzani nchini Tanzania ACT Wazalendo kimeeleza kuwa mkuu wa tawi la vijana wa chama hicho Abdul Nondo ambaye wanadai alitekwa jana na vikosi vya usalama, alipatikana usiku katika fukwe za jiji la Dar Es Salaam akiwa na majeraha na sasa amelazwa hospitalini.
Chama hicho kilisema Nondo alikamatwa katika kituo cha mabasi alipokuwa akirejea kutoka mkoani Kigoma mashariki mwa Tanzania. Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara Isihaka Mchinjita ameandika kwenye ukurasa wa X kuwa ukatili wanaopitia vijana, utaligeuza taifa hilo kuwa uwanja wa fujo na visasi.
Hayo yanajiri siku chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi za serikali za mitaa ambao baadhi ya vyama vya upinzani vinataka ufutwe kutokana na kasoro nyingi zilizoshuhudiwa.