1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Kagame ashinda uchaguzi wa rais kwa karibu asilimia 100

Sylvia Mwehozi
16 Julai 2024

Rais Paul Kagame wa Rwanda amejizolea asilimia 99 ya kura, kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliofanyika siku ya Jumatatu huku wapinzani wawili pekee wakishindwa kupata hata asilimia moja ya kura.

https://p.dw.com/p/4iMWm
Paul Kagame
Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi, saa saba baada ya vituo vya kura kufungwa, yanaonyesha kuwa Kagame amepata asilimia 99.15 ya kura, ikiwa ni zaidi ya asilimia 98.79 alizopata katika uchaguzi uliopita. Mgombea wa chama cha Democratic Green Party Frank Habineza amepigiwa kura kwa asilimia 0.53 na mgombea mwingine huru Philippe Mpayimana, amepata asilimia 0.32 baada ya asilimia 79 ya kura kuhesabiwa.

Akizungumza katika makao makuu ya chama tawala cha Rwandan Patriotic Front (RPF), Kagame mwenye umri wa miaka 66, aliwashukuru Wanyarwanda kwa kumpatia muhula mwingine wa miaka mitano mamlakani.

Alisema kuwa "ama kuhusu takwimu hizi, hata kama ingekuwa asilimia 100, hizi sio namba tu. Takwimu hizi zinadhihirisha uaminifu na hilo ndio muhimu zaidi," alisema Kagame.

 Philippe Mpayimana | Paul Kagame | Frank Habineza
Wagombea waliochuana na Paul Kagame(katikati), Philippe Mpayimana |(kushoto) na Frank Habineza(kulia)Picha: AFP

Baadhi ya Wanyarwanda walikuwa na matarajio yafuatayo;

 "Baadhi ya vijana hawana ajira. Matarajio yangu kwa rais ajaye wa nchi yetu ni rais atakayetengeneza nafasi za ajira kwa ajili ya vijana wa kike na kiume. Hilo litaboresha maisha ya vijana"

"Ninachotamani kwa kiongozi wetu ajaye, kwa sababu amefanya mengi, natamani aendeleze kile ambacho amekifanya, kwamba wanyarwanda waendelee katika mwelekeo sahihi, katika nyanja zote. Mambo mengi yamefanyika. Leo hii, sisi kama wanawake tuna sauti".Rwanda: Kagame kurejea madarakani kwa muhula wa nne?

Katika taarifa yake, Tume ya uchaguzi ya Rwanda, imedai kuwa kwa "ujumla mchakato wa uchaguziumefanyika katika mazingira salama na ya uwazi kwa Wanyarwanda wanaoishi nje na ndani ya nchi."

Matokeo hayo ya uchaguzi wa Jumatatu hayakuwa ya kutiliwa shaka kamwe, wakati Rais Kagame akiwa amelitawala taifa hilo dogo la Afrika Mashariki kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.

Wanyarwanda wamchagua rais na wabunge

Kiongozi huyo anasifiwa kwa kulijenga upya taifa lililokumbwa na taharuki baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, lakini pia anashutumiwa kutawala katika mazingira ya hofu na kuchochea ukosefu wa utulivu katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa mnamo Julai 20 na matokeo ya uhakika ni Julai 27.

Wapinzani wa Kagame: Wafahamu wagombea wawili wanaochuana na Kagame

Zaidi ya Wanyarwanda milioni 9, walijiandikisha kupiga kura zao, huku kinyang'anyiro cha urais kikifanyika kwa wakati mmoja na uchaguzi wa wabunge kwa mara ya kwanza.

Kagame alishinda kwa zaidi ya asilimia 93 ya kura mwaka 2003, 2010 na 2017, alipowashinda kwa urahisi wapinzani wake wawili. Amesimamia marekebisho ya katiba yenye utata ambayo yalifupisha mihula ya urais kutoka miaka saba hadi mitano, hatua inayomwezesha kiongozi huyo wa Rwanda kutawala hadi mwaka 2034.