1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame ashinda kwa kishindo uchaguzi Rwanda

Sekione Kitojo
5 Agosti 2017

Kiongozi aliyeko madarakani nchini Rwanda Paul Kagame amekamilisha  ushindi mkubwa katika  uchaguzi  wa  rais ambao unampatia muhula wa tatu madarakani, akirefusha  utawala wake  wa miaka  17 sasa akiwa madarakani.

https://p.dw.com/p/2hjWt
Ruanda Wahlen- amtierender Präsident Paul Kagame (RPF)
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/G. Dusabe

Kagame amesifiwa  kimataifa  kwa  kuiongoza nchi  hiyo katika  kipindi cha  amani  na ukuaji  wa  haraka  wa  uchumi katika  taifa  hilo  la  Afrika  ya kati  tangu  mauaji  ya  kimbari ya  mwaka 1994, wakati Watutsi  wanaokadiriwa  kufikia 800,000 pamoja  na  Wahutu waliochukua  msimamo  wa  wastani walipouwawa  kikatili. Lakini pia  amekumbana  na shutuma kali zinazoongezeka  kwa  kile  ambacho  wakosoaji  na  makundi  ya  haki  za binadamu  yanasema  ni ukiukaji  mkubwa  wa  haki  za  binadamu , ukandamizaji  wa vyombo  huru  vya  habari na  kukandamiza  pia  upinzani  wa  kisiasa.

Ruanda Präsidentschaftswahlen Kampagne Präsident Paul Kagame
Ras Paul Kagame akishangiria pamoja na wafuasi wake ushindi wa uchaguzi mjini KigaliPicha: Reuters/J. Bizimana

Wakati  asilimia  80 zimekwisha  hesabiwa , kiongozi  huyo  mwenye umri  wa  miaka  59 mpiganaji  wa  zamani  wa  chini  kwa  chini  amekwishapata  asilimia 98.66, amesema katibu  mktendaji  wa  tume  ya  taifa  ya  uchaguzi Charles Munyaneza alipokuwa akizungumza  na  waandishi  habari.

"Tunatarajia  kwamba  hata  kama  tutapata asilimia  100 ya  kura , hakutakuwa  na mabadiliko  yoyote,"amesema .

Tume  hiyo  inatarajia  watu  waliojitokeza  kupiga  kura  kufikia  asilimia  90  katika  taifa  hilo la  Afrika ya  kati  lenye  wakaazi wapatao milioni  12 mara  taarifa  kamili  zitakapojitokeza, katika  uchaguzi ambao mgombea pekee  wa  upinzani  alikuwa  mmoja, Frank Habineza  , na  mwingine  wa  kujitegemea.

Ruanda Präsidentschaftswahlen Frank Habineza
Mgombea wa upinzani wa chama cha Kijani Frank HabinezaPicha: Reuters/C. Uwiringiyimana

Kazi itakayofuata ni kuimarisha uchumi

Kagame, ambae alipiga  kura  yake katika  kituo  cha  kupigia  kura  mjini  Kigali  cha Rugunga mapema  jana  Ijumaa, alisema  atafanyakazi  kuendeleza  ukuaji  wa  uchumi katika  taifa  hilo dogo.

"Huu  ni  muhula  mwingine  wa miaka  7 kushughulikia  masuala  ambayo  yanawaathiri Wanyarwanda  na  kuhakikisha  kwamba  tunakuwa  kweli Wanyarwanda  ambao wanaendelea  kiuchumi," alisema  katika  hotuba  iliyotangazwa  moja  kwa  moja  katika televisheni.

Ruanda Präsidentschaftswahlen Wahllokal in Kigali
Kura zikihesabiwa katika uchaguzi mkuu wa rais nchini RwandaPicha: Reuters/J. Bizimana

Chini ya  utawala  wake , baadhi  ya  wapinzani  wameuwawa  baada  ya  kukimbilia uhamishoni, katika  kesi  ambazo  bado  hazija patiwa ufumbuzi.

Serikali  inakana  kuhusika  kwa  njia  yoyote  ile.

Kagame, kamanda  ambaye  ameliongoza  jeshi  la  waasi  wa  Kitutsi  kuingia  nchini Rwanda  na  kufikisha  mwisho  mauaji  ya  kimbari  ya  mwaka  1994, amepiga  marufuku matumizi ya  maneno  ya  kikabila baada  ya  kuwa  rais.

Alishinda  uchaguzi  uliopita  mwaka  2010 kwa  asilimia  93 ya  kura  na  wakati  wa  kipindi cha  kampeni  kwa  ajili ya  muhula  wa  miaka  7 , alisema  anatarajia  ushindi  wa  kishindo.

Habineza , ambae hadi  sasa  amepata  asilimia  0.45 ya  kura zilizokwisha hesabiwa , ameahidi  kuunda  mahakama  ya  kuwashitaki tena  wapinzani  ambao hukumu  zao zilizopitishwa  na  mahakama  za  Rwanda  zimekosolewa kama zimekuwa  na  hamasa  za kisiasa.

Ruanda Präsidentschaftswahlen Wähler in Kigali
Mpiga kura akitia kura yake katika kasha la kura tarehe 04.08.2017 mjini KigaliPicha: Reuters/J. Bizimana

Mgombea  mwingine  ambaye  anaonekana  kuwa  nae ni  mpinzani , Diane Rwigara , aliondolewa  na  tume  ya  uchaguzi  licha  ya  msisitizo wake  kuwa  alitimiza mahitaji  yote ya kugombea.

"Kwangu  mimi  nauona  uchaguzi  huu  kama  wa  mbio za  mtu  mmoja. Mimi  sikwenda kupiga  kura," amesema  mtu  mmoja  mjini  Kigali ambaye  hakutaka  aliomba  jina  lake lihifadhiwe.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri : Isacc Gamba