Kamala: Marekani itaisaidia kanda ya ASEAN mzozo wa Myanmar
6 Septemba 2023Ahadi hiyo ya msaada wa Marekani imetolewa na Makamu wa Rais wa taifa hilo Kamala Harris wakati akiwahutubia viongozi wakuu wa mataifa ya ASEAN.
Viongozi hao wanakutana kwenye mji mkuu wa Indonesia, Jakarta, tangu siku ya Jumanne kwa mkutano wa kilele ambao moja ya ajenda kubwa ni hali dhaifu ya kisiasa nchini Myanmar.
Kamala Harris amesema Marekani itaendelea kuwashinikiza majenerali nchini Myanmar kukomesha matendo ya kikatili, kuwaachia huru watu waliokamatwa kiholela na kuirejesha nchi hiyo kwenye mkondo wa demokrasia.
Amesema Washington haitaitupa mkono kanda ya ASEAN na itazidi kuyaimarisha mahusiano yaliyomea vizuri kwa kuisaidia kutimiza wajibu wake.
Myanmar ilitumbukia kwenye mgogoro Februari mwaka 2021 baada ya jeshi kutwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi.
Waliuangusha utawala wa kiraia wa Aung San Suu Kyi na kumweka kizuizini. Tangu wakati huo taifa hilo limo kwenye hali ya machafuko na vurumai isiyo mfano.
Mzozo wa Myanmar bado ni pasua kichwa kwa kanda ya ASEAN
Majenerali wanatumia mabavu kuwakandamiza wale wanaowapinga wakivishambulia vijiji kwa ndege za kivita na ngome za wapiganaji wasiowaunga mkono.
Makundi ya haki za kiraia yanasema hujuma hizo zimekuwa pia zikiwaua raia wasio na hatia kwa kuyalenga maeneo ya umma kama shule, masoko na hospitali.
Katika siku ya kwanza ya mkutano wa ASEAN siku ya Jumanne, viongozi wa kanda hiyo walitoa tamko la kuwataka manajerali kusitisha hujuma hizo.
Pia walielezea kufadhaishwa na kutopiga hatua kwa makubaliano ya kusitisha machafuko nchini humo uliojumuisha mpango wa kuanzisha mazungumzo ya ngazi ya taifa kuyatafutia ufumbuzi masuala yanalota migawanyiko.
Mpango huo wa vipengele vitano ulifikiwa baina ya kanda ya ASEAN na watalawala wa kijeshi wiki chache baada ya mapinduzi ya mwaka 2021.
Makamu wa Rais wa Marekani pia aliugusia mpango huo kwenye hotuba yake na Washington inauunga mkono na inapigia upatu utekelezaji.
Waziri Mkuu wa China asema Jumuiya ya ASEAN lazima ijiepushe na kuchagua upande
Mapema hii leo viongozi wa ASEAN walifanya mikutano na viongozi wengine wa dunia ikiwemo China.
Waziri Mkuu wake Li Qiang aliihimiza kanda hiyo kujiepusha kuchagua upande katika ulimwengu wa sasa unaokabiliwa na mivutano hususan kati ya Beijing na Marekani.
Qiang pia alizungumzia umuhimu wa kutatua mivutano kwa njia za kiungwana kuepusha kile amekitaja kurejea kwa enzi ya vita baridi.
Viongozi wa Canada, Korea Kusini na Waziri Mkuu wa Canada nao waliwahutubia viongozi wa ASEAN. Mkutano huo unahitmishwa leo.
Ajenda nyingine zilizogubika mjadala ni usalama wa mtandao, haki za binadamu, mzozo kwenye bahari ya kusini mwa China na ushirikiano wa kiuchumi.