Kamanda wa Kikurdi atangaza usitishaji vita Syria
11 Desemba 2024Kamanda wa kikosi cha wapiganaji wa Kikurdi kinachodhibiti eneo kubwa la Kaskazini Mashariki mwa Syria, amesema wamefikia makubaliano ya kusitisha vita katika eneo linalokaliwa na jamii kubwa ya waarabu la Manbji.
Kamanda wa kikosi cha SDF Mazloum Abdi amesema makubaliano hayo yamefikiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Uturuki, chini ya usimamizi wa Marekani na kuongeza kwamba wapiganaji wa kikosi cha SDF wataondolewa kwenye eneo hilo la Manbji hivi karibuni.
Makubaliano hayo yametangazwa leo baada ya hapo jana kutangazwa kwa kiongozi mpya wa serikali ya mpito ya Syria, Mohammed al Bashir ambaye amewatolea mwito wasyria waliokimbilia nje warejee nyumbani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameitaka serikali hiyo mpya kutimiza ahadi zake za kuheshimu kikamilifu haki za walio wachache na kutowa msaada wa kiutu kwa watu wote wenye uhitaji.