1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamishna wa magereza Kenya ashitakiwa

Admin.WagnerD18 Novemba 2021

Kamishna Mkuu wa Magereza nchini Kenya Wycliffe Ogalo amefunguliwa mashitaka baada ya rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi. hatua hii inafuatia magaidi watatu kutoroka gerezani mapema wiki hii.

https://p.dw.com/p/438j5
Kenia Präsident Uhuru Kenyatta
Picha: PPS-presidential press service

Kamishna Mkuu wa Magereza nchini Kenya Wycliffe Ogalo ametiwa nguvuni muda mfupi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kufutwa kazi kwake. Ogalo na mafisa wengine wakuu wa gereza lenye ulinzi mkali la Kamiti walikamatwa na kuhojiwa na maafisa wa kitengo cha upelelezi. Hayo yanajiri baada ya magaidi watatu kutoroka gereza hilo hapo juzi Jumanne.

Uamuzi wa kuwakamata maafisa hao wakuu wa magereza unajiri muda mfupi baada ya Rais Kenyatta kukutana na maafisa wakuu katika wizara ya Usalama wa Taifa wakiongozwa na waziri Fred Matiangi. Kwenye kikao hicho cha faragha, ilifichuliwa kuwa, maafisa wa magereza walitepetea katika utendaji kazi wao.

Ogalo amehudumu kwa muda mrefu katika serikali na alikuwa amehudumu kwenye cheo hicho kwa kipindi cha miaka miwili. Alichukua nafasi Isaya Osugo ambaye aliacha sifa ya kutekeleza mabadiliko kadha kwenye idara hiyo. Rais Kenyatta amemteua na kushuhudia kamishna mpya Brigadia mstaafu John Kibaso Warioba akila kiapo cha utendajikazi katika ikulu ya Nairobi.

Alisema "Niko katika mchakato wa kuchukua nafasi ya mtangulizi wangu, kwa sasa hayo ndio naweza kuwafahamisha.”

Kenia Garissa Universität Anschlag Trauer
Miongoni mwa wanafunzi waliookolewa kwenye shambulizi la kigaidi kwenye chuo kikuu cha Garissa Aprili 2015Picha: picture-alliance/dpa/D.Irungu

Hata hivyo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Idara ya kuwaajiri Maafisa wa Polisi imekanusha habari za kutiwa nguvuni kwa kamishna Ogalo, ikisema ni za kupotosha. Idara hiyo imesema hatua iliyochukuliwa ilikuwa ya kupisha uongozi mpya. Hata hivyo wakili wa Ogola, Assa Nyakundi alithibitisha kuwa, Ogalo aliachiliwa baadaye bila ya masharti kutoka kwa makao makuu ya Idara ya Upelelezi.

Nyakundi alisema kuwa mteja wake alitakiwa kuondoka bila ya maelezo yoyote. Kuondoka kwa Ogalo, ni nafuu kwa baadhi ya maafisa wa kitengo hicho cha kurekebisha tabia, hasa katibu mkuu Zeynab Mohammed ambaye hawajakuwa wakielewana naye, na kuongeza kuwa "Brigedia mstaafu Warioba, ni mtumishi wa umma mwenye uzoefu wa siku nyingi na tunaamini anaweza kuifanya kazi hii”.

Maafisa tisa wa magereza wanazuiliwa rumande kufuatia kutoroka kwa magaidi hao waliokuwa wanatumika vifungo vya ugaidi.  Uhuru pia aliamuagiza Matiang'i kutumia kila njia kuwakamata magaidi hao waliotoroka kwenye gereza la Kamiti. Maafisa waliohusika kuwatorosha magaidi hao pia wameonywa kuwa watawajibika, pindi watakapopatikana. Aidha maafisa waliokuwa kazini, wakati wa tukio hilo wametakiwa kusimamishwa kazi ama kuhamishwa.

Magaidi hao walitoroka baada ya kuchimba shimo na kuruka uzio wa gereza hilo lenye ulinzi mkali kwa kutumia Kamba. Musharraf Abdalla Akhulunga anayejulikana kwa jina lengine Zarkarawi, Mohammed Ali Abikar and Joseph Juma Odhiambo anayejulikana pia kama Yusuf hawajapatikana hadi kufikia sasa huku idara ya upelelezi ikitoa shilingi milioni 60 za Kenya kwa maelezo ambayo yatasaidia kukamatwa kwao.   

Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW, Nairobi