KAMPALA : Museveni kuwapa waasi n’gombe 10
22 Desemba 2006Rais Yoweri Museveni wa Uganda atapeleka n’gombe dume 10 kwa waasi wa LRA kwa ajili ya X’masi ili kuonyesha nia njema ya serikali ya Uganda katika mazungumzo ya amani kwa mkuu mwenye shaka wa waasi hao Joseph Kony.
N’gombe hao watapelekwa pamoja na zawadi nyenginezo kwa waasi hao waliokusanyika kwenye kambi mbili kusini mwa Sudan nchi ambayo ni mwenyeji wa mazungumzo hao ya amani yenye lengo la kurudisha utulivu kaskazini mwa Uganda kulikoathirika na vita.
Msemaji wa Rais Museveni Tamale Murundi amesema kile anachokifanya rais huyo ni kumhakikishia Kony kwamba anataka kutimiza ahadi yake ya kumpa msamaha.
Museveni ameahidi kutowa msamaha kamili kwa Kony ambaye pamoja na makamanda wanne waandamizi wa LRA wanashtakiwa kwa uhalifu wa vita na Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu iwapo makubaliano ya amani yatafikiwa.
Kony ana hofu kwamba mazungumzo hayo ya amani ni hila ya kumkamata na kumkabidhi kwa mahkama hiyo ya kimataifa.