Kanisa Katoliki: CENI itangaze matokeo ya kweli
4 Januari 2019Kanisa hilo sasa linaitaka tume ya uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo ya kweli.
Wito huu wa baraza la kitaifa la makanisa nchini Congo CENCO umekuja baada ya tume ya uchaguzi kutangaza kwamba italazimika kuchelewa kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Jumapili kutokana na hitilafu za kimitambo.
Padri Donatien Nshole ni msemaji na Katibu Mkuu wa baraza hilo. "Data tulizozipata kutoka vituo vya kupigia kura zinathibitisha kuchaguliwa kwa mgombea mmoja kama rais wa Jamhuri hii," alisema Padri Donatien. "Kwa hiyo, tunaitaka tume ya uchaguzi CENI, kama taasisi inayounga mkono demokrasia, kuchapisha matokeo ya uchaguzi katika njia ya uwajibikaji huku ikiheshimu ukweli na haki," aliongeza kiongozi huyo wa dini.
Marekani inataka CENI itangaze matokeo sahihi
Baraza hilo la makanisa linasema lilikuwa na waangalizi zaidi ya 40,000 kote nchini humo kuangalia jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa na kulingana na padri Nshole, maafisa wake walibaini mapungufu katika uchaguzi huo. Lakini amesema kuwa mapungufu hayo hayakuwa makubwa kiasi cha kumuathiri yule aliechaguliwa na raia wa Congo.
Marekani imetaka matokeo sahihi yatangazwe na kusema yeyote atakayekwenda kinyume na demokrasia ya nchi hiyo atawekewa vikwazo. Marekani pia imeitaka serikali ya Congo kuufungua mtandao wa intaneti na kuondoa vikwazo kwa vyombo vya habari.
Shirika la utangazaji la Ufaransa RFI ambalo lina wasikilizaji wengi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo linasema mwandishi wake Florence Morice alilazimika kuondoka nchini humo usiku wa Alhamis baada ya kibali chake cha kufanya kazi kufutiliwa mbali. Uongozi wa Congo kupitia waziri wa mawasiliano Lambert Mende unalituhumu shirika hilo kwa kuleta utata kwa kutangaza matokeo yasiyo rasmi madai ambayo shirika lenyewe limekanusha.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya kikao Ijumaa
"Ni muhimu kufahamu kwamba chini ya sheria za Congo, ni CENI na CENi pekee yenye mamlaka ya kuandaa uchaguzi na kutangaza matokeo," alisema Lambert Mende.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa litafanya mkutano wa faragha leo kujadili huo uchaguzi wa Congo. Ufaransa ndiyo iliyouitisha mkutano huo, wakati ambapo mataifa yenye nguvu duniani yanasubiri matokeo ya uchaguzi huo.
Tume ya uchaguzi imepanga kutangaza matokeo ya awali Jumapili kisha matokeo kamili yatangazwe Januari 15 na rais aliyechaguliwa aapishwe siku tatu baadae.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga