Kansela Angela Merkel ziarani Mumbai
31 Oktoba 2007Kansela Angela merkel anaendelea na ziara yake ya siku nchini India.Hii leo ameutembelea mji mkuu wa kibiashara Mumbai ambako ametilia mkazo umuhimu wa mikopo midogo ya kujiendeleza.
Mtu anaweza kuilinganisha sura ya mambo na hali ya usiku na mchana.Kwa muda wa siku mbili nzima kansela Angela Merkel alikua na mazungumzo ya kisiasa katika mji mkuu wenye majengo ya tangu enzi za ukoloni au katika hoteli ya fakhari ya taj Mahal.
Hii leo sura ya pili ya India ndiyo iliyojitokea-maeneo ya madongo poromoka ya mji wenye wakaazi milioni 16 yameenea mpaka karibu na uwanja wa ndege wa Bombay au Mumbai kama unavyojulikana hivi sasa.Mumbai una sura mbili- ile ya utajiri na ya ufukara uliokithiri nchini India.
Katika mji mkuu huyo wa kiuchumi na fedha wa India-Mumbai,kansela Angela Merkel aliitembelea kwanza benki ya maendeleo ya NABARD na kupatiwa maelezo kuhusu mradi mkubwa kabisa duniani wa mikopo midogo midogo.Mradi huo unazinufaisha familia milioni 40.
Leo jioni kansela Angela merkel amepangiwa kuzungumza na gavana wa jimbo la Maharashtra pamoja pia na wawakilishi wa sekta ya kiuchumi.
Katika benki ya NABARD kansela Angela Merkel alikutana na wakinamama 15 waliounda shirika la kujisaidia kuweza kupata mikopo rahisi kununulia zana,mbegu au kugharimia masomo ya watoto wao.
Kote nchini India kuna mashirika milioni mbili na laki tisaa ambalo kila moja lina wanaachama wasiopungua 13.Wanapatiwa mikopo ,kilas mmoja yuro 85 kwa riba ya karibu asili mia 12.Zamani mikopo kama hiyo ilikua ikilipiwa riba ya asili mia 300.
Kansela Angela Merkel amevutiwa sana na mradi huo.Amekumbusha mikopo midogo midogo ndio kiini cha misaada ya maendeleo ya Ujerumani kwa India.
“Nimefurahishwa sana na kuvutiwa sana kuona jinsi mradi huu unavyotekelezwa.”Amesema kansela Angela Merkel.
Shirika la Ujerumani la ushirikiano wa kiufundi-GTZ linasimamia miradi hiyo nchini India tangu miaka minane iliyopita.
Hadi sasa yuro bilioni moja nukta nane zimetolewa kugharimia mradi huo.Asili mia 90 ya waliokopeshwa ni wakinamama.
Kansela Angela Merkel amearifiwa na wenyeji wake kila amwanamme mmoja kati ya watano waliopatiwa mkopo huo amefanikiwa kujikwamua toka hali ya umaskini.
Baada ya mazungumzo yake katika benki ya NABARD,wakinamama 15 wanaunda shirika la kujisaidia wamemualika kansela Angela Merkel aitembelee tena India.”Utakuja kijijini kwetu,la sivyo tutakuja sote kijijini kwenu” mmojawapo amesema.
Kansela Angela Merkel anatarajiwa kurejea nyumbani kesho alkhamisi.