Kansela Merkel amaliza ziara yake nchini India
1 Novemba 2007Kansela Angela Merkel anamaliza ziara yake ya siku nne nchini India hii leo mjini Bombay.Ametetea haja ya kuwa na ushirikiano wa aina moja pamoja na India na China.
Mnamo siku hii ya mwisho ya ziara yake nchini India,kansela Angela Merkel amekutana na wawakilishi wa kidini na jamii za wachache mjini Bombay.
Kansela Angela Merkel amesema ziara yake hii ya kwanza nchini India imefanikiwa pakubwa.Kansela Angela Merkel ameongeza kusema tunanukuu:”Kwa mtazamo wangu mie ziara hii ya India imeupa msukumo mkubwa uhusiano kati ya Ujerumani na India” mwisho wa kumnukuu kansela Merkel aliyeitaja India kua ni nchi yenye “fursa chungu nzima.”Umuhimu wa India ulimwenguni utazidi kukua miaka inayofuatia.
Kansela Angela Merkel amesema mazungumzo imara ya kisiasa,ushirikiano wa kiuchumi na misaada ya ,maendeleo ndio mhimili wa ushirrikiano wa kimkakati kati ya Ujerumani na India.
Ameahidi misaada zaidi ya Ujerumani kwa India-naiwe katika kupatiwa familia mikopo midogo midogo ya kujiendeleza au katika juhudi za kulinda mazingira.
Kansela Angela Merkel amesisitiza haja ya kuwaona wahindi wote wakifaidika sawa na neema ya kiuchumi ya nchi hiyo.
“Katika mapambano dhidi ya umasikini kote ulimwenguni,panahitajika makaazi zaidi katika miji mikubwa mikubwa,huduma bora za maji na afya pamoja na fursa ya kupata elimu.Mustakbal wa ubinaadam unategemea mambo hayo” amesisitiza kansela Angela Merkel katika sherehe za kutolewa tuzo ya benki mashuhuri ya Ujerumani- Deutsche Bank kwa miradi ya kuimarisha maisha katika miji”.
Mkurugenzi mkuu wa Deutsche Bank Josef Ackermann ametoa zawadi hiyo yenye thamani ya dala laki moja,kwa miradi miwili ya maendeleo katika miji mjini Bombay.
Kansela Angela Merkel anasema kuna fursa kubwa ya kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na India,akisisitiza haja ya kua na ushirikiano wa aina moja pia pamoja na India na China.
“Hatubidi kuzigonganisha kwa namna yoyote ile nchi hizi mbili”amesema kansela Angela Merkel mbele ya waandishi habari mjini Bombay.
Kabla hajaondoka Bombay kurejea nyumbani hii leo,kansela Angela Merkel amepangiwa kuuzuru mradi wa kuwajumuisha walemavu katika maisha ya kila siku ya jamii.
Ziara ya kansela Angela Merkel nchini India ni ya tatu barani Asia,baada ya kuzitembelea jamhuri ya umma wa China na Japan.