Kansela Merkel awasili India
31 Mei 2011Jana usiku, Iran kwa muda mfupi wa masaa mawili ilifunga anga yake na kuizuwia ndege iliokuwa imemchukuwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kutokea Ujerumani kwenda India kuruka katika nga ya nchi hiyo. Ndege hiyo, chapa ya Airbus, ilibakia ikizunguka katika anga ya Uturuki kwa masaa mawili, na baada ya zaidi ya saa moja ya mashauriano, zikiwaingiza wakuu wa Uturuki na na wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani, ndege hiyo ndipo iliporuhusiwa kuendelea na safari yake juu ya anga ya Iran kuelekea New Delhi.
Bibi Merkel alizuilika pale alipokuwa akisafiri jana usiku , na hivyo kuchelewa kwenda kukutana na waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, na pia rais wa India, Pratibha Patil mjini New Delhi.
Kitendo hicho cha Iran kilimfanya waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, kutoka tamko lifuatalo:
"Kuzuiliwa kwa safari ya Kansela wa Ujerumani ni jambo lisilokubalika kabisa, ni kutoonesha heshima kuelekea Ujerumani, jambo ambalo hatulikubali. Nimemwita balozi wa Iran mjini Berlin, na tutaweka wazi kabisa kwamba kwenda kinyume na namna hiyo dhidi ya safari za kimataifa za ndege kutoka Ujerumani hakutakubaliwa klwa namna yeyote ile."
Sababu ya kucheleweshwa ndege hiyo hakujulikani bado, lakini ndege ya pili ya serekali ya Ujerumani iliokuwa imembeba mawaziri wanne wa serikali ya Bibi Merkel na wajumbe wengine haijazuiliwa, iliruka juu ya anga ya Iran bila ya matatizo hadi New Delhi.
Bibi Merkel, akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na Bwana Manmohan Singh, alikataa kuzungumzia kwa undani ya mkasa huo. Alisema amefurahi kwamba amewasili salama, na kila kitu kilikwenda vizuri; wao wamewasili kufanya mashauriano na India, na hilo ndio jambo muhimu.
"Naamini balozi ataulizwa, ataombwa atoe maelezo, hivyo ni sawa kumwita na kumuomba atoe maelezo; si suala la kukasirika, ni suala la kutaka ufafanuzi."
Duru za serikali ya Ujerumani zilisema ndege hiyo aliokuwemo Kansela Merkel iliruhusiwa tu kuingia katika anga ya Iran baada ya ujiingizaji mkubwa wa kidiplomasia mjini Berlin na Tehran. Hapo kabla, ruhusa ya ndege hiyo kuruka katika anga ya Iran ilitolewa na haijulikani kwanini baadae iliondoshwa.
Waziri mdogo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani anatazamiwa kukutana leo na balozi wa Iran mjini Berlin kupata maelezo.
Katika mkutano wa waandishi wa habari huko New Delhi, Bibi Merkel alisema nchi yake itakuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa juu ya Afghanistan mwishoni mwa mwaka huu, na ilikuwa inatafuta kuweko masikilizano baina ya makundi katika nchi hiyo, ikiwa makundi hayo yatatimiza masharti, kama vile kuachana na matumizi ya nguvu.
Ujerumani pia imeripotiwa kuwa inasaidia kupatanisha kwa siri ili yafanyike mazungumnzo ya moja kwa moja baina ya Marekani na Wataliban wa Afghanistan.
Pia huko India, Kansela Merkel atashawishi India inunue ndege za chapa Eurofighter zinazotengenezwa na mchanganyiko wa makampuni ya Ulaya, zabuni inayogharimu Rupia za India bilioni 12. Ujerumani ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa India katika Ulaya, na biashara kati ya nchi hizi mbili inatazamiwa kufikia Euro bilioni 20 ifikapo mwakani.
Kuhusu nani wa kukamata wadhifa wa mkuu mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, nafasi ambayo Ujerumani inashikilia ikamatwe na Mfaransa, Bibi Christine Legard, waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, amesema uendeshaji wa taasisi za kimataifa unahitaji uambatane na ukweli halisi wa hali ya mambo ya sasa. Alisema mtu aliye bora kabisa, bila ya kujali uraia wake, ateuliwe kwa wadhifa huo .
Mwandishi: Miraji Othman/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo