1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel nchini India

5 Oktoba 2015

Ujerumani na India zimesaini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara,hatua ambayo inatarajiwa kuyarahisishia makampuni ya Ujerumani kuendesha biashara katika taifa hilo la Asia.

https://p.dw.com/p/1GikM
Angela Merkel na Narendra Modi mjini New-Delhi
Angela Merkel na Narendra Modi mjini New-DelhiPicha: R. Schmidt/AFP/Getty Images

Ujerumani na India zimesaini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara,hatua ambayo inatarajiwa kuyarahisishia makampuni ya Ujerumani kuendesha biashara katika taifa hilo kubwa linaloshikilia nafasi ya tatu kiuchumi barani Asia. Makubaliano hayo yametangazwa katika wakati ambapo Kansela Angela Merkel yuko ziarani nchini humo.

Makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili ni ya kwanza ya aina yake na yanafanyika wakati waziri mkuu wa India Narendra Modi akitafuta njia za kuwavutia wawekezaji wa kigeni kujikita nchini Mwake hatua ambayo inakusudiwa kuimarisha uwekezaji katika sekta ya viwanda pamoja na uzalishaji wa nafasi za ajira.

Makubaliano hayo yatayahakikishia makampuni ya Ujerumani kupata nafasi ya kuwasiliana mojakwa moja na utawala wa India kuhusiana na masuala ya kibiashara hatua ambayo itayasaidia kuvuka mtandao mkubwa wa sheria nyingi ambazo mara nyingi ni kizuizi katika juhudi za kibiashara. Waziri wa biashara wa India Amitabh Kant amebaini kwamba kwa mujibu wa makubaliano hayo India itafuatilia kila mwezi masuala yote ya kibiashara kwa ajili ya makampuni ya Ujerumani.

Kansela Merkel akisaini kitabu cha wageni akiwa New-Delhi
Kansela Merkel akisaini kitabu cha wageni akiwa New-DelhiPicha: R. Schmidt/AFP/Getty Images

Kufuatia makubaliano hayo waziri huyo wa biashara wa India ameongeza kusema kwamba nchi yake imeweka matarajio makubwa kwasababu huo ndio mwanzo wa ukuaji wa muda mrefu wa hali ya kiuchumi kwa taifa hilo.Kansela Angela Merkel kwa upande mwingine atatarajiwa kumuhimiza waziri mkuu Modi kurudi kwenye meza ya mazungumzo kuhusiana na suala la makubaliano ya biashara huru na Umoja wa Ulaya,makuabaliano ambayo yamekwama tangu India ilipojiondoa kwenye mazungumzo mwaka huu.

Halikadhalika Ujerumani imesema India inahitaji kuondoa vikwazo vingi vinavyozunguka suala zima la biashara ikiwa ni pamoja na kuwepo mtandao mkubwa wa sheria zinazohusu biashara,hali mbaya ya Miundo mbinu pamoja na rushwa.Waziri wa mammbo ya nje wa Ujerumani Frank WalterSteinmeir ametoa kauli hiyo iliyochapishwa katika gazeti la Hindustani leo.

Steinemeier amesema ili India ipate ushirikiano zaidi wa kibiashara na Uwekezaji wa makampuni ya kijerumani inabidi ichukue hatua ya kuondoa vikwazo vingi vilivyopo.Ziara ya siku tatu ya Kansela Angela Merkel nchini India inalenga zaidi kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ulinzi,nishati mbadala pamoja na biashara nyingine kati ya nchi hizo mbili.

Mkutano wa kilele wa kibiashara unaowajumuisha wawakilishi katika sekta ya biashara kutoka pande zote mbili umepangiwa kufanyika leo wakati Merkel na Modi wakipangiwa kuwa na mkutano na wakuu wa makampuni huko Bangalore hapo kesho Jumanne.Merkel ameongozana katika ziara hiyo na ujumbe mzito wa mawaziri akiwemo waziri wa mambo ya nje Steinmeeir pamoja na wakuu wa makampuni ya Ujerumani.Tangu mwaka 1991 hadi Februari mwaka huu uwekezaji wa moja kwa moja wa Ujerumani nchini India umefikia thamani ya dolla bilioni 8.25.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/dpa/afp

Mhariri:Josephat Charo