Kansela Merkel ziarani Ugiriki
9 Oktoba 2012Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, yuko Ugiriki leo (09.10.2012) kufanya mazungumzo na viongozi wa taifa hilo kuhusiana na msaada wake, unaolenga kuiepusha Ugiriki na kufilisika na hivyo kubakia mwanachama wa kanda inayotumia sarafu ya euro. Mjini Athens, raia wenye hasira wamemkaribisha Merkel kwa maandamano wakipinga mpango huo wa kubana matumizi.
Vikosi vya ulinzi vinaweka doria mjini Athens, ili kuhakikisha utulivu na usalama unatawala wakati wote Angela Merkel akiwa katika mazungumzo na viongozi wa serikali hiyo, ziara ambayo ni ya kwanza tangu kuvunjika kwa mazungumzo ya mzozo huo wa madeni unaoikabili Ugiriki.
Polisi watapakaa Athens kulinda usalama
Zaidi ya polisi 7,000 wakiwemo wadunguaji wametapakaa katika viunga vya mji mkuu huo ili kulinda barabara itakayotumiwa na msafara wa kiongozi huyo wa Ujerumani.
Polisi imeweka marufuku ya kufanyika maandamano katika maeneo mengi katikati ya mji huo mkuu. Merkel anatarajiwa kuwepo mjini hapo kwa saa sita mfululizo.
Hatahivyo, taarifa zinapasha kuwa marufuku hayo hayahusiani na maandamano yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi na yale yanayoratibiwa na vyama vya upinzani. Merkel anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu Antonis Samaras.
Serikali ya mseto inayoongozwa na Samaras inahitaji uhuru zaidi katika kutekeleza mpango huo wa kubana matumizi, kama inavyotakiwa na wakopeshaji wa kimataifa wa Ugiriki katika kurejesha fedha za dhamana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la Kathimerini, Samaras anatumai kupata kibali cha Kansela Merkel kwa mpango wa kubana matumizi ambao si mkali sana, ambao Ugiriki unaujadili pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa, Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya.
Ziara ya Merkel Ugiriki yatafsiriwa tofauti tofauti
Ujio huu wa Kansela Merkel nchini Ugiriki unatafsiriwa kama ishara njema ya nia yake thabiti ya kuona nchi hiyo inayokabiliwa na madeni bado ikibaki kuwa mwanachama wa kanda inayotumia sarafu ya euro.
Kwa upande mwingine, Wagiriki wengi wanamlaumu Merkel kwa kutaka hatua kali za kubana matumizi kama kigezo cha kuipatia nchi yao dhamana. Ikumbukwe kwamba uchumi wa Ugiriki umekuwa ukidorora kwa muda wa miaka mitano huku ikiomba muda zaidi wa kutekeleza mpango wa kubana matumizi ili kujimudu kiuchumi.
Waziri Mkuu Samaras anataka kupunguza makato hayo, sawa na euro bilioni 13.5, ili kuepuka kuathiri mishahara ya wafanyakazi wa umma sanjari na mafao ya uzeeni. Wachunguzi wa mambo wanadai kuwa makato hayo yataifanya Ugiriki kuendelea kudorora kiuchumi kwa mwaka wa sita itakapofika mwaka 2013.
Kansela Merkel anatarajiwa pia kukutana na Rais Karolos Papoulias na wawakilishi wa viwanda vya Ujerumani na Ugiriki.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\ DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman