1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz afanya ziara ya kushtukiza mjini Kyiv

2 Desemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amefanya ziara ya kushtukiza nchini Ukraine hivi leo, ili kuthibitisha uungaji mkono wa Berlin kwa Kyiv katika vita vyake dhidi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4ndlx
Ukraine Kiev 2024 | Ziara ya Kansela Scholz
Kansela Scholz atoa wito wa juhudi za kijeshi lakini pia za kidiplomasia katika harakati za kuvimaliza vita Ukraine, katika namna ambayo italinda uhuru wa Ukraine.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Kiongozi huyo ambaye amedhihirisha mshikamano wake na Ukraine, amesema katika mkutano wake na Rais Volodymyr Zelensky, atatoa ahadi ya msaada wa ziada wa kijeshi wenye thamani ya dola milioni 680 utakaowasilishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Ziara ya Scholz inafanyika huku vikosi vya Ukraine vikipata pigo katika mstari wa mbele wa vita kutokana na mashambulizi makubwa ya Moscow ambayo yamesababisha uharibifu kwenye miundombinu ya nishati ikiwemo gridi ya taifa ya umeme.

Sholz anazuru Ukraine wakati taarifa zikisema, wanajeshi wa Ukraine walioko msitari wa mbele wameelemewa na vita.

Na kwa upande mwingine, Urusi inashambulia miundombinu ya nishati na kuongeza mashaka kwa watu wa nchi hiyo inayoingia kwenye majira ya baridi kali.

Lakini pia wasiwasi wa Marekani kuondoa msaada wa kijeshi kwa taifa hilo mara baada ya Rais mteule Donald Trump kuingia madarakani mwezi Januari mwakani, nacho ni kitisho kingine kinachoweza kuongeza ugumu zaidi kwa upande wa Ukraine inayopigana na Urusi kwa zaidi ya siku 1,000 sasa.