1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KANU yamteua Gideon Moi kuwania urais Kenya 2022

Shisia Wasilwa
30 Septemba 2021

Wajumbe wa Chama cha KANU nchini Kenya wameafikiana kwa kauli moja kumteua Gideon Moi, kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao. Gideon ni mwanaye aliyekuwa rais hayati mzee Daniel Arap Moi

https://p.dw.com/p/416Fr
Kenia Nairobi | Gideon Moi  und weitere
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Hatua ya Gideon kujitosa katika kinyang'anyiro hicho kinazidisha fumbo katika kiti hicho kinachomezewa mate na wagombea kadhaa nchini Kenya.

Ukumbi wa Bomas, maarufu kwa mikutano mikuu ya kisiasa nchini Kenya, ulijaa wajumbe waliokuwa na mavazi mekundu yenye nembo ya jogoo ya chama cha KANU katika kongamano kuu la taifa la chama hicho. Wajumbe hao 3000 waliotoka katika majimbo yote 47 ya taifa la Kenya, walianza kufika mapema na asubuhi.

Pendekezo la kumteua Gideon Moi liliwasilishwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Nick Salat, na kupokelewa kwa shangwe na hoi hoi. Huku akiwa amevalia suti nyeusi na shati jekundu, Gideon alipokewa kwenye jukwaa na mkewe Zahra aliyekuwa amevalia buibui ya rangi nyeusi.

”Lakini tuseme ukweli, kama chama tumepitia nyakati ngumu, ila katika historia ya miaka 60 kujitolea kwetu  na upendo kwa taifa, hukuwezi kutikiswa, kwa miaka hiyo yote KANU kinaweza kutajwa kuwa chama cha Taifa.”

Kwa kipindi cha miaka 20 tangu Uhuru Kenyatta aliyekuwa mgombea urais wa chama cha KANU kushindwa mwaka 2002, kwenye uchaguzi mkuu, chama hiki hakijawahi kugombea tena kiti cha urais. Iwapo Gideon atavumilia mawimbi ya siasa hadi mwakani, ataandikisha historia ya chama hicho.

Gideon Moi
Gideon Moi kugombea urais kwa tiketi ya KANU 2022Picha: Khalil Senosi/AP/dpa/picture alliance

Hata hivyo kama ishara ya muungano mpya wa siasa unaonukia, viongozi wa One Kenya Alliance-OKA, akiwemo Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga walihudhuria hafla yenyewe. Wote wakisema kuwa wako tayari kushirikiana na Gideon siku zijazo. Hii ina maana, gani? swali hilo linajibiwa na Felix Ochieng ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa. "Gideon na Raila wameshakubaliana. Tatizo ni viongozi wengine wa One Kenya Alliance, Mudavadi, Kalonzo na Wetangula ambao hawajakubali, hivyo wakishakubaliana nadhani wataunda mrengo mkubwa utakaomenyana na UDA.”

Moi sasa atakabiliana na wagombea wengine akiwemo Naibu rais William Ruto ambaye ametangaza kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.  Wajumbe wa Chama cha KANU, kilichobuniwa na baba wa taifa Mzee Jomo Kenyatta mwaka 1960, taifa lilipokuwa likijiandaa kupata uhuru kwa mkoloni, wamechangamkia hatua ya Gideon, wakivitaka vyama vingine kuunga mkono azma ya Gideon. Rachel Njenri ni mjumbe. "Ni chama kinachojali kila mtu, vijana kina mama na pia ni chama cha zamani.”

Gideon ambaye ni kitindamimba wa hayati mzee Moi ameliambia kongomano la taifa la chama chake kuwa, hivi karibuni ataelezea ilani yake na jinsi ya kuliwezesha taifa la Kenya kukabiliana na donda dugu la ufisadi.

Wakati huo huo Wakenya wanaendelea kuelezea hisia zao baada ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi na Mipaka Ezra Chiloba, kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya. Mamlaka ya Mawasiliano ina dhima kuu kwenye uchaguzi mkuu, kwani husimamia mitandao yote ya intaneti nchini pamoja na data zote. Chiloba alinyoshewa kidole cha lawama kwa kuvuruga uchaguzi mkuu ulionadaliwa mwaka 2017.