1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Karibu watu 56 wauawa katika machafuko nchini Sudan

16 Aprili 2023

Karibu raia 56 wameuawa nchini Sudan, kufuatia makabiliano kati ya wanajeshi wa Sudan na kikosi maalumu cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, RSF ambayo hayajashuhudiwa tangu mapinduzi ya 2021.

https://p.dw.com/p/4Q9KK
Wanajeshi wa RSF wakilinda eneo ambako kiongozi wao Jenerali Dagalo anahudhuria mkutano wa hadhara.
Mataifa mbalimbali ulimwenguni yameeleza hofu yao kufuatia kuibuka kwa mapigano nchini Sudan ambayo hayajashuhudiwa tangu mwaka 2021.Picha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Mamia ya watu pia wameripotiwa kujeruhiwa, hali inayoibua wasiwasi wa kimataifa.

Kulingana na Kamati Kuu ya madaktari nchini Sudan makumi ya wanajeshi wa usalama pia wameuawa, lakini idadi yao haijajumuishwa na hii iliyotolewa mapema leo na kuongeza kuwa karibu watu 600 wamejeruhiwa.

Mapigano yameibuka mapema leo kufuatia mvutano mkali wa hivi karibuni kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake Mohammed Hamdan Dagalo, ambaye ni kamanda wa vikosi hivyo vya RSF.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito wa kusitisshwa mapigano mara moja, huku Muungano wa mataifa ya Kiarabu nao ukikutana hii leo kwa mkutano wa dharura kwa ajili ya Sudan

Pande hizo mbili zinazolaumiana kwa kuanzisha mapigano, zote zinadai kuidhibiti miji muhimu.