Kasheshe ya Özil na Trump Magazetini
24 Julai 2018Jazba hazijatulia bado baada ya aliyekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani, mzaliwa wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki, Mesut Özil kutangaza anajitoa katika timu ya taifa ya kabumbu na kulalamika hathaminiwi na kwamba anabaguliwa tangu na shirikisho la kabumbu DFB mashabiki mpaka na vyombo vya habari. Maoni yanatofautiana katika nyanja zote za jamii, kuanzia miongoni mwa wanasiasa, wanamichezo, na bila ya shaka wahariri. Gazeti la "Emder Zeitung" linahisi hoja za Özil ni kisingizio tu: Gazeti linaendelea kuandika: "Cha kuzingatia ni kwamba Mesut Özil amezaliwa na kukulia Ujerumani, ni mtoto wa mto Ruhr anaetokana na familia yenye asili ya Uturuki. Amepata fursa zote humu nchini, na kupatiwa mafunzo ya kuwa mwanasoka wa ngazi ya juu kwa hivyo kuwa mtu mwenye kipato cha juu na kipenzi cha vyombo vya habari. Wale anaowatupia lawama za ubaguzi, yaani shirikisho la kabumbu la DFB ndio waliochangia pakubwa katika kuchaguliwa kwake kuwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa. Kile anachoshindwa kukivumilia Özil ni ule ukweli kwamba hashangiriwi tena kama shujaa seuze kama mwanasoka wa kipekee. Kama kweli yuko hivyo mbona ameshindwa kudhihirisha hilo nchini Urusi. Kujiuzulu kwake kumetangulia uamuzi wa kumwacha kando na hilo lingetokea hata bila ya picha pamoja na Erdogan."
Suala la watu kuishi pamoja ni tete
Hofu zimeenea kisa cha Özil kisije kikakorofisha juhudi za kuishi pamoja jamii mbali mbali nchini Ujerumani. Gazeti la "Badische Neuste Nachrichten" linaandika: "Kadhia ya Özil haistahiki kushawishi juhudi za Ujerumani za kuhimiza kuishi pamoja watu wa jamii tofauti humu nchini. Mada hiyo ni tete na yenye kupandisha jazba pia. Hakuna njia sahihi katika mada hiyo. Sawa na katika dimba ukweli unapodhihirika uwanjani, ndipo katika maisha ya kawaida pia ukweli unadhihirika miongoni mwa majirani, shule, mitaani na katika uhusiano kati ya mtu na mtu."
Trump anyunyizia mafuta katika cheche za moto
Mvutano umepamba moto kati ya Marekani na Iran. Hofu zimeenea vita vya maneno visije vikageuka ukweli wa mambo. Gazeti la "Oberhessische Presse" linaandika. Malumbano yameripuka katika njia panda kati ya Iran na Marekani. Rais Donald Trump ananguruma na kumtahadharisha rais wa Iran Hassan Ruhani. Na ili aweze kuelewa amekusudia nini, anamtumia risala ya twitter kutoka ikulu ya white House iliyoandikwa kwa herufi kubwa: "Usisubutu kushindana na mie". Kuna kila sababu ya watu kuingiwa na hofu kwasababu haipiti wiki kabla ya Donald Trump kuja na mepya ; mara auwekee suala la kuuliza uhusiano pamoja na jumuia ya kujihami, mara aseme ataiotoa nchi yake. Mara aukaripie Umoja wa ulaya na kuutaja kuwa adui.... mradi vitisho havishi.....
.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef