1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya NSA na goli hewa magazetini

29 Oktoba 2013

Kashfa ya kusikilizwa mawasiliano ya simu ya kansela Angela Merkel na kisa cha goli hewa lililoipatia pointi tatu za bure timu ya dimba ya Bayer Leverkusen ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari .

https://p.dw.com/p/1A7i3
Kansela Angela Merkel akizungumza na rais Barack Obama wa Marekani Juni 6 mwaka huu huko Los Cabos,MexicoPicha: picture-alliance/dpa

Kashfa ya kusikilizwa mawasiliano ya simu ya mkononi ya kansela Angela Merkel na kisa cha goli hewa lililoipatia pointi tatu za bure timu ya dimba ya Bayer Leverkusen ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani.

Tuanze lakini na kashfa inayozidi kupandisha ghadhabu miongoni mwa wanasiasa na wananchi nchini Ujerumani: Kashfa ya kusikilizwa kwa siri mawasiliano ya simu ya viongozi wa serikali na wale wa kisiasa wa humu nchini, wakitanguliwa na kansela Angela Merkel. Miito imehanikiza kutaka kamati maalum ya bunge iundwe kuchunguza kashfa hiyo. Gazeti la Rhein-Necker la mjini Heidelberg linaandika:

Kinachopangwa na walinzi wa mazingira die Grüne na Social Democratic kwa ridhaa ya vyama ndugu vya kihafidhina vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU, ni korti yenye kutoa maneno mengi bila ya kupata maelezo yoyote kwa sababu hakuna si shirika la upelelezi la NSA na wala si rais Barack Obama, seuze mfichua siri mtoro Edward Snowden atakaeweza kuitwa kama shahidi kujieleza. Kamati ya uchunguzi ambayo maelezo yake itayapata kutoka mtu watatu, yaani maelezo ya kile watu walichokisikia au kilichosemwa tu, haiwezi kutoa matokeo ya kuridhisha.

Protest in den USA NSA Überwachung
Malalamiko dhidi ya upeleleziPicha: Getty Images

Visa vyote vya upelelezi vichunguzwe

Gazeti la mji wa kaskazini -"Hannoversche Allgemeine" linataka uchunguzi huo usiishie pekee katika kashfa ya upelelezi ya shirika la NSA. Gazeti linaendelea kuandika:

Kamati ya uchunguzi ambayo hatimaye vyama ndugu vya CDU/CSU vimeridhia iundwe, haipaswi kuishia katika kuchunguza kashfa ya kusikilizwa mawasiliano ya simu za mkononi za kansela tu. Inabidi, kwa ushirikiano pamoja na kamati kama hizo za bunge la Ulaya ambazo tayari zimeshaanza kukutana, ichunguze harakati zote za idara za upelelezi (hata zile za kutoka Ujerumani) na kusaka ufumbuzi wa maana. Ufumbuzi huo uzingatie mbali na mfumo wa kinga dhidi ya upelelezi, kubuniwa mtandao wa pamoja wa nchi za Ulaya. Shuhguli za mtandao zinabidi zifanyike chini ya mwamvuli wa Ulaya. Kinga halisi itaweza tu kupatikana kwa msaada wa injini ya kutafuta habari - Servern na Cloud itakayodhaminiwa na sheria za Ulaya.

Goli hewa lapita mahakamani

Baada ya kashfa ya NSA, inafuata kadhia ya goli hewa lililoingia katika mchuano wa wiki iliyopita wa ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga kati ya Bayer Leverkusen na Hoffenheim. Mahakama ya michezo mjini Frankfurt imeamua: goli lililopita ndani ya tundu wavuni na kuingia langoni ni halali. Pambano hilo kwa hivyo halitarudiwa. Bayer Leverkusen wamejipatia pointi tatu za bure. Gazeti la Westdeutsche la mjini Düsseldorf linaandika:

Fußball Bundesliga 10. Spieltag Leverkusen Augsburg Kiessling 26.10.2013
Goli hewa la Stefan Kießling lililoipatia timu ya Bayer Leverkusen pointi tatu za burePicha: Thorsten Wagner/Bongarts/Getty Images

Kitu pekee kinachoweza kumaliza udhia ni ushahidi wa kanda ya video. Kanda hiyo ingemuepushia zaidi Stefan Kießling lawama za kila aina. Kwa namna hiyo, tangu yeye mpaka kufikia msimamizi wa pambano hilo wangesalimika.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanadspresse

Mhariri: Josephat Charo