1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya simu yamuangusha mkuu wa polisi Uingereza

Mohamed Dahman18 Julai 2011

Kashfa ya kunasa mazungumzo ya simu ya kampuni News Corporation imemgharimu wadhifa wake mkuu wa polisi nchini Uingereza na kuzusha hofu Waziri Mkuu David Cameron, anavyolishughulikia suala hilo.

https://p.dw.com/p/11yPK
Mkuu wa Polisi wa London, Sir Paul Stephenson
Mkuu wa Polisi wa London, Sir Paul StephensonPicha: AP

Sakata hilo lililomuangusha mkuu wa polisi wa Uingereza limesababisha kukamatwa kwa mhariri wa zamani wa gazeti la News of the World nchini Uingereza na kupelekea kupomoromoka kwa hisa za kampuni hiyo nchini Australia.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amefupisha ziara yake ya kibishara ya siku nne barani Afrika kwa siku mbili kutokana na kuongezeka kwa shinikizo lenye kumtaka kiongozi huyo wa chama cha Consevartive kuishughulikia kashfa hiyo ambayo imedhoofisha imani ya wananchi wa Uingereza kwa polisi, vyombo vya habari na viongozi wa kisiasa.

Alipoulizwa kwa nini Cameron ameamuwa kuendelea na ziara yake Afrika Kusini na Nigeria wakati kashfa hiyo ikizidi kutokota nchini Uingereza, msemaji wa Cameron amesema Waziri Mkuu ana dhima na majukumu mbali mbali ya kutimiza, mojawapo likiwa ni suala la uchumi na kukuza biashara ya Uingereza.

Paul Stephenson, mkuu wa polisi wa jiji la London, amejiuzulu jana kutokana na madai kwamba maafisa wa polisi wamekuwa wakipokea fedha kutoka gazeti la kampuni hiyo na haikuchukuwa hatua za kutosha kuchunguza madai ya kunasa mazungumzo ya simu yalioanza kuibuka tokea mwaka 2005.

Mmiliki wa News of the World, Rupert Murdoch
Mmiliki wa News of the World, Rupert MurdochPicha: dapd

Kujiuzulu kwake kumetokana na habari kwamba aliwahi kukaa katika eneo la chemchemi la kifahari ambapo Neil Wallis, mhariri wa zamani wa gazeti la News of the World, kitovu cha kashfa hiyo, alikuwa afisa uhusiano.

Wallis ambaye alikuwa pia ameajiriwa na polisi kama mshauri, alikamatwa wiki iliopita kutokana na kuhusika na kashfa hiyo ya kunasa mazungumzo ya simu.

"Sikalii wadhifa wowote ule katika ulimwengu wa uandishi wa habari duniani. Sina habari juu ya ukubwa wa kitendo hiki cha aibu na jinsi kinavyochukiza katika uteuzi wa wahanga wake, mambo ambayo hivi sasa yanajitokeza na jinsi ilivyowafikia watu wa ngazi ya juu." Amesema Paul Stephenson wakati akitowa taarifa ya kujiuzulu kwake hapo Jumapili.

Murdoch, tajiri mwenye kumiliki vyombo vya habari, mzaliwa wa Australia, imebidi alifunge gazeti lake la News of the World ambalo lilikuwa kitovu cha kashfa hiyo ya kutega mazungumzo ya simu na imebidi pia aachane na mpango wa dola bilioni 12 wa kuinunuwa kampuni ya matangazo ya satalaiti yenye kuzalisha faida kubwa ya BSkyB.

Wakati kashfa hiyo ikipamba moto, hisa za kampuni ya habari News Corp nchini Australia zimeshuka kwa asilimia 7.6 hadi kuwa dola 14.53, ambacho ni kiwango cha chini kabisa kuwahi kufikiwa tokea mwezi wa Julai mwaka 2009 na punguzo la asilimia 7.4 kwa kampuni hiyo wakati masoko ya hisa yalipomaliza biashara yake nchini Marekani. Hiyo inamaanisha kutakuwepo na hasara ya mtaji wa soko wa dola bilioni tatu wakati biashara itakapoanza tena nchini Marekani.

Rebekah Brooks mkuu wa zamani wa kitengo cha magazeti cha kampuni ya News Corp ameachiwa kwa dhamana baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kunasa mawasiliano ya simu na rushwa.

Gazeti la News of the World ambalo lilitowa toleo lake la mwisho wiki iliopita linadaiwa kunasa mazungumzo ya simu takriban 4,000 ikiwa ni pamoja na yale ya Milly Dowler msichana mwenye umri wa miaka 13 aliyeuwawa na kuzusha shutuma zilizomlazimisha Murdoch kulifunga gazeti hilo na kuachana na mpango wa kununuwa kampuni ya BskyB.

Mwandishi: Mohammed Dahman/RTRE
Mhariri: Miraji Othman